May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchango wa mbunge Lambart wa CHADEMA watikisa wabunge

Na Mwandishi Wetu, Mwandishi Wetu,TimesMajira, OnlineDodoma

MCHANGO wa Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Agnesta Lambart, kuhusu hofu yake kutokana na Idara ya Uhamiaji kutakiwa kubadilishwa na kuwa jeshi kamili umetikisa Bunge, hali iliyofanya baadhi ya wabunge kulazimika kusimama kumpata taarifa ambazo hakukubaliana nazo.

Wakati akichangia muswada uliopelekwa na Serikali Bungeni, jijini Dodoma leo kuhusu marekebisho ya sheria mbalimbali namba 5 ya mwaka 2021, mbunge huyo ametoa angalizo juu ya mambo mawili kabla ya kupitisha sheria ya kufanya Idara ya Uhamiaji kuwa jeshi kamili.

“Mheshimiwa Spika kabla ya uamuzi kupandisha Idara ya Uhamiaji kuwa jeshi kamili kufikiwa ni lazima tujiulize mambo makuu mawili, ikiwemo suala zima la mahusiano ya kimataifa na mataifa mengine,” amesema Lambart na kuongeza;

“Mheshimiwa Spika najaribu kufikiria mtalii au mwekezaji au kule ubalozini mtu anakuja kutafuta nyaraka au anakuja nchini anakutana na uhamiaji wamekamilika itaonekanaje huko nje!”

Lambart ambaye ni Mjumbe wa Katiba na Sheria, amesema Ibara ya 28 inapendekeza katika kifungu kidogo cha 4 cha Sheria ya Uhamiaji sura ya 54 kuitambua Idara ya Uhamiaji kuwa ni Jeshi kamili bila kubadilisha jina.

Amesema anatambua nia njema ya Serikali juu ya jambo hilo, lakini yapo mambo kadhaa ambayo wao kama wabunge wanatakiwa kuyatafakari kabla hawajapitisha sheria hiyo.

Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Agnesta Lambart

Lambart amesema suala la majeshi ni suala la kikatiba, hivyo wanapokuwa wanapitisha sheria hiyo, hawana budi kuhakikisha sheria hiyo haiendi kukinzana na Katiba.

“Mheshimiwa Spika, kuanzisha au kufuta jeshi jipya au kulipa hadhi, jambo hili linatakiwa kuangaliwa kwa kina kwa maana ya Katiba ya nchi, kwani bila hivyo tunaweza kujikuta tunachanganya Katiba pamoja na sheria ya nchi,” amesema Lambart.

Ameongeza kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano haitambui Idara ya Uhamiaji kuwa miongoni mwa majeshi katika nchi yetu, huku akitolea mfano Ibara ya 147 kifungu kidogo cha nne cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Katiba haitambui kabisa Idara ya Uhamiaji, hivyo unapokuwa unaletwa muswada kama huu tunaweza tukaipa Idara ya Uhamiaji hadhi ya jeshi,” amesema na kuongeza;

“Sasa mheshimiwa Spika unaposema unakwenda kupandisha Idara ya Uhamiaji kuipa hadhi ya kuwa jeshi kamili, wakati Katiba Ibara 147 kifungu kidogo cha 4 haitambui. Ina maana ili tuweze kuipandisha hadhi Idara ya Uhamiaji kuwa jeshi kamili yapo mambo ya kufuata na kuzingatia.”

Amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano inamtambua Rais kama Amiri Jeshi Mkuu na Katiba inasema Amiri Jeshi Mkuu pale anapoona kwamba kuna hali ya uhatari, hali ya udharura juu ya jambo fulani la kijeshi, atatoa kitu kinachoitwa Hati Idhini .

“Mheshimiwa Spika, ukirejea kwenye taarifa hiyo ya Kamati imeongelea vizuri kwamba Hati Idhini kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu ilipashwa kupelekwa kwao ili ipate kuwa mwongozo wa Bunge,” ameisema Lambart.

Wakati akiendelea kuchangia, Spika alimtaka mchangiaji kutaja kifungu cha Katiba kinachotaja Hati Idhini. Hata hivyo, aliomba kuendelea kuchangia akiongelea hicho kitu kinachoitwa Hati Idhini kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu.
Amesema wao kama Kamati ya Katiba na Sheria wakati wanajadiliana pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, walihoji kwamba wanataka kupata Hati Idhini iweze kuwaongoza.

Wakati akichangia mbunge huyo na kutokana na uzito wa hoja alizokuwa, wabunge kadhaa wa CCM walisimama na kumpa taarifa ambazo hakukubaliana nazo.

Miongoni mwa waliosimama na kumpata taarifa mbunge huyo ni pamoja Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akitoa mifano baadhi ya nchi ikiwemo Uingereza akisema Uhamiaji ni jeshi na wanatumia silaha na kwamba ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

“Marekani, Uhamiaji ni jeshi, India, Austeria uhamiaji ni jeshi, kwa hiyo watatuonaje, watatuona tunafanana na wao,” amesema Simbachawene.

Wakati akitaka kuendelea kuchangia kengele ya pili iligongwa, hivyo Spika hakupa nafasi ya kumalizia mchango wake kama alivyokuwa akiomba.