January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Nkasi,aitaka serikali magonjwa yasiyoambukiza kutibiwa bure

Na Doreen Aloyce,Timesmajira online, Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Nkasi Kaskazini Aida Khenani ameiomba Serikali kuja na njia mbadala ya kusaidia wananchi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kutibiwa bila malipo.

Mbunge huyo ameyasema hayo katika viwanja vya Bunge alipokuwa akizungumza katika kuelekea kupitishwa kwa bajeti ya afya kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo ameeleza kuwa afya ndio kila kitu katika maisha.

Amesema kuwa serikali ikiondoa kodi ya matibabu katika magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari,saratani,kifafa pamoja na ajali itasaidia kuokoa maisha ya watanzania wengi.Pia amesema kuwa kwa magonjwa yasiyoambukiza gharama ni kubwa na ngumu kwa mtanzania wa kawaida kuweza kumudu kulipa matibabu hayo.

“Yapo magonjwa ambayo yanaweza kumtokea mtu yoyote mfano ajali inaweza kukukuta hata ukiwa nyumbani,suala la ajali ni lazima serikali ilitazame kwa kina kwani kuna ajali ambazo ni muhimu ione namna ya kuweza kuwasaidia watanzania,”amesema Mbunge huyo.

Katika hatua nyingine amemtaka Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kuweka wazi ugonjwa wa Corona kutokana na maneno ya chinichini yaliyopo mtaani.

“Juzi nimefanya utafiti wangu binafsi nimeenda duka moja la dawa nimekutana na wananchi kibao wanaulizia dawa ya Corona jambo limeleta mashaka kwa nini serikali haifunguki tujue hali ilivyo huko hospitalini,”alihoji Mbunge Khenani.