May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya CRDB yapata faida sh. bil. 351 mwaka 2022

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Arusha

BENKI ya CRDB imekuwa ikiimarika kila mwaka kwa kuongeza faida na thamani ya hisa zake, ambapo kwa mwaka 2022, baada ya kodi, imeweza kupata faida ya sh. bilioni 351 ikilinganishwa na sh. bilioni 36 kwa mwaka 2017, na hilo ni ongezeko la asilimia 875.

Na kutokana na ukuaji huo wa faida, thamani ya hisa imepanda sokoni, ambapo baada ya CRDB kutangaza matokeo yao ya hesabu za fedha hivi karibuni, hisa imepanda hadi sh. 510, ambapo mwaka 2017 bei ya hisa moja ya Benki ya CRDB ilikuwa sh. 90, na hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 567 ndani ya miaka mitano.

Hayo yalisemwa Mei 16, 2023 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari na Benki ya CRDB jijini Arusha kwa ajili ya kuujulisha umma mambo yaliyofanywa na benki hiyo kwa kipindi kilichopita, lakini pia kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB Mei 20, mwaka huu, ukitanguliwa na semina kwa wanahisa Mei 19, mwaka huu na shughuli za kijamii.

“Mageuzi thabiti yanathibitishwa na taarifa zetu za fedha zinazoonesha, katika miaka mitano iliyopita, utendaji wa benki umekuwa ukiimarika licha ya changamoto kadhaa zilizotokea kwenye mazingira ya ufanyaji biashara hasa zikichangiwa na janga la UVIKO-19 na vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine.

“Faida Baada ya Kodi imeongezeka kufika sh. bilioni 351 mwaka 2022 ikilinganishwa na sh. bilioni 36 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 875.
Na kutokana na ukuaji huo wa faida, thamani ya hisa imepanda sokoni, ambapo baada ya CRDB kutangaza matokeo yao ya hesabu za fedha hivi karibuni, hisa imepanda hadi sh. 510, ambapo mwaka 2017 bei ya hisa moja ya Benki ya CRDB ilikuwa sh. 90, na hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 567 ndani ya miaka mitano” alisema Dkt. Laay.

Dkt. Laay alisema kukua kwa uwekezaji wa Benki nje ya mipaka ambapo hivi karibuni wamefanikiwa kupata leseni ya kufungua kampuni tanzu Benki ya CRDB Tawi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), uwekezaji huo wa nchini DRC unatarajiwa kuongeza thamani kwa wanahisa wao kama ambavyo imekua nchini Burundi.

Alisema kuwa ukuaji huu ni viashiria vya utendaji makini unaoonesha mageuzi thabiti katika utendaji wa benki hiyo na uwekezaji wa wanahisa wa CRDB, kama ambavyo kaulimbiu ya Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa mwaka huu inavyosema ‘Mageuzi Thabiti’.

“Ufanisi nilioueleza hapo juu umepatikana wakati tukihitimisha utekelezaji wa Mpango Mkakati wetu wa muda wa kati wa miaka mitano kuanzia mwaka 2018 mpaka mwaka 2022, na sasa tumeanza kuufanyia kazi Mpango Mkakati mpya utakaotupeleka mpaka mwaka 2027” alisema Dkt. Laay.

Dkt. Laay alisema baadhi ya mambo ambayo yatatakiwa kuidhinishwa yapo katika taarifa ya mwaka ikiwamo taarifa ya Wakurugenzi, na pendekezo la gawio ambapo mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi imependekeza ni gawio la sh. 45 kwa hisa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 kulinganisha na gawio la sh. 36 lililotolewa mwaka jana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela, alisema benki hiyo inayomilikiwa kwa mfumo hisa, inatambua jukumu muhimu ambalo wanahisa wake wanalo katika kuimarisha utendaji wa benki na kuamua mustakabali wa sasa na baadaye.

Nsekela alisema nguvu ya Benki ya CRDB ipo katika uwezo wa pamoja wa wanahisa wao. Maoni yao yanawawezesha kukabiliana na changamoto, kutumia fursa, na kutoa ukuaji endelevu kila mara. Hilo limewasaidia, kujenga msingi imara na thabiti ambao juu yake wameendelea kushuhudia mafanikio makubwa.

“Ukiachilia kuwa ni matakwa ya kisheria, Benki yetu ya CRDB inachukulia kwa umuhimu sana Mkutano Mkuu wa Wanahisa (AGM). Mkutano huu umekuwa jukwaa muhimu kwa Menejimenti, Bodi na Wanahisa wote kwa pamoja kujadiliana na kutolea maamuzi masuala muhimu ya maendeleo ya benki yetu.

“Bodi yetu ya Wakurugenzi ikiwa chombo cha uwakilishi wa Wanahisa katika kuisimamia vyema benki yetu kwa manufaa ya wanahisa, imekuwa ikifanya kazi nzuri ikiwamo kuhakikisha Mkutano Mkuu unafanyika na wanahisa wanapata haki yao ya msingi ya kufanya maamuzi, na kuwasilisha maoni kwa ajili ya kuboresha utendaji wa benki yao” alisema Nsekela.

Nsekela alisema wakati wa Mkutano Mkuu, mambo mengi hujadiliwa ikiwemo mafanikio yaliyofikiwa katika vipindi vilivyopita, na mipango ya kimkakati inayopangwa kutekelezwa katika siku za usoni. Hiyo imekuwa fursa muhimu kwa wanahisa kushiriki kikamilifu katika kujenga mwelekeo wa baadaye wa Benki yao ya CRDB.

Nakuongeza kuwa kwa mwaka huu, Wanahisa watapata nafasi ya kufahamu juu ya mkakati mpya wa biashara wa muda wa kati wa miaka mitano 2023/2027, ambao Bodi ya Wakurugenzi iliupitisha mwaka jana mwishoni.

“Mkakati huu ambao umebebwa na kaulimbiu ya Mageuzi Thabiti unalenga katika kuimarisha utendaji wa benki yetu na kuifanya kuwa kinara katika kila nyanja katika soko yaani Undisputed leader. Hivyo basi ushiriki wa wanahisa katika Mkutano Mkuu utasaidia na wao kujua namna gani wanaweza kutoa mchango wao katika kufanikisha malengo yaliyowekwa na kuifanya benki yetu kuwa bora zaidi” alisema Nsekela.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay (katikati) akizungumza kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari na Benki ya CRDB uliofanyika Mei 16, 2023 jijini Arusha. Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto), Katibu wa Kampuni ya Benki ya CRDB John Rugambo (kushoto), Mjumbe wa Bodi ya Benki ya CRDB nchini Burundi Kahumbya Bashige (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation Tully Mwambapa (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto), akizungumza kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari na Benki ya CRDB uliofanyika jijini Arusha Mei 16, 2023. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay (katikati), Katibu wa Kampuni ya Benki ya CRDB John Rugambo (kushoto), Mjumbe wa Bodi ya Benki ya CRDB nchini Burundi Kahumbya Bashige (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation Tully Mwambapa (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).
Maofisa wa Benki ya CRDB nchini, wakishiriki Mkutano wa Waandishi wa Habari na Benki ya CRDB uliofanyika jijini Arusha Mei 16, 2023. (Picha na Yusuph Mussa).
Maofisa wa Benki ya CRDB nchini, wakishiriki Mkutano wa Waandishi wa Habari na Benki ya CRDB uliofanyika jijini Arusha Mei 16, 2023. (Picha na Yusuph Mussa).
Maofisa wa Benki ya CRDB nchini, wakishiriki Mkutano wa Waandishi wa Habari na Benki ya CRDB uliofanyika jijini Arusha Mei 16, 2023. (Picha na Yusuph Mussa).