April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Masanja akabidhi mizinga ya nyuki,majiko ya gesi kwa wanawake wajasiriamali.

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amekabidhi mizinga ya nyuki 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)Sengerema, mitungi ya gesi 150 yenye thamani ya shilingi milioni 12,750,00 na fedha taslimu shilingi milioni 4.5 kwa wanawake wajasiriamali wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

Hafla hiyo imefanyika Machi 28, 2023 katika Ukumbi wa Wajasiriamali Wilayani Sengerema ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe. Senyi Ngaga.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Masanja amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ina mkakati wa kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu ya mkaa na kuni, hivyo ugawaji wa majiko ya gesi ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kutunza mazingira.

Amesema nishati ya gesi itawasaidia wajasiriamali hao kuepukana na magonjwa ya mapafu na matatizo ya macho yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa katika kupikia.

“Serikali imefanya utafiti na kugundua takribani watu elfu 33 kila mwaka wanapata changamoto ya magonjwa ya mapafu, upofu na kuwa na macho mekundu inayotokana na moshi wa mkaa pamoja na kuni” Mhe. Masanja ametahadharisha.

Amesema Serikali inaendelea kuelimisha wananchi kwamba matumizi sahihi na salama ni kutumia nishati safi ikiwa pamoja na nishati ya gesi na jua.

Kuhusu mizinga ya nyuki, Mhe. Masanja amewataka wanawake hao kutafuta eneo maalum la kuiweka mizinga hiyo kwa ajili ya kuanzisha biashara ya urinaji wa asali, ambapo pia utasaidia upatikanaji wa nta na maziwa ya nyuki.

Aidha, ameishukuru Kampuni ya ORYX kwa kutoa mitungi ya gesi bure itakayowasaidia wajasiriamali hao kujiongeza kipato.

Mhe. Masanja pia ametoa fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 4,500,000 ambapo kila mjasiriamali alipata shilingi elfu 30,000 kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali hao kuendelea kujinunulia gesi .

Hafla hiyo imehudhuriwa na wananchi Wajasiriamali wadogo wadogo, vijana na wenye walemavu.