



Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Kilombero mkoani Morogoro Abubakar Asenga, amepokea vifaa vya msaada kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa, kwa ajili ya kuwasaidia wananchi walioathiriwa na mafuriko yaliyolikumba jimbo hilo hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya mafuriko, Asenga amewapa pole wananchi wa maeneo yaliyoathirika zaidi ,ya Michenga, Lumemo na Lipangalala, akieleza kuwa safari hii kiwango cha maji kimekuwa kikubwa zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma, hali iliyosababisha madhara makubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.
Amesema takribani kaya 100 zimeathirika, huku idadi ya watu waliofikiwa na athari za mafuriko ikikadiriwa kuwa kati ya 15,000 hadi 16,000. Hata hivyo, amebainisha kuwa hakuna kifo kilichoripotiwa hadi sasa kutokana na maafa hayo.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, msaada uliotolewa unajumuisha magodoro 75, mablanketi 100 na vyandarua 100 na mahindi tani 10 yakiwa njiani kupelekwa jimboni humo huku akisisitiza kuwa vifaa hivyo vya dharura vitasaidia kupunguza adha kwa wananchi waliopoteza makazi na mali zao.
Asenga ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba kwa hatua za haraka walizochukua kuhakikisha misaada inawafikia wahanga wa mafuriko.
Aidha, amepongeza juhudi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ,wananchi na kamati ya maafa kwa kazi kubwa ya kuwaokoa wananchi waliokuwa hatarini, akibainisha kuwa mchango wao umechangia kwa kiasi kikubwa kuepusha upotevu wa maisha.
Mbali na misaada hiyo, Mbunge huyo amesema ofisi yake inaendelea kutafuta unga kwa ajili ya kuwasaidia wananchi waliokumbwa na janga hilo, ili kukidhi mahitaji ya chakula kwa kipindi hiki kigumu.
Katika hatua nyingine, Asenga amesema wabunge wanaendelea kuisimamia Serikali kutekeleza mpango wa kufukua mito,mabwawa na kuweka matuta hatua inayolenga kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa sasa, vifaa vya msaada vinaendelea kusafirishwa kuelekea Jimbo la Kilombero, huku Mbunge Assenga naye akielekea jimboni humo kwa ajili ya kushiriki moja kwa moja katika kuwafariji na kuwasaidia wananchi wake.

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT