April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mbunge apatikana na corona, wagonjwa wafikia 254

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepata maabukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID 19).

Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, aliwaambia wabunge jana jijini Dodoma, kwamba pamoja na taratibu walizojiwekea kukabiliana na ugonjwa huo, lakini wamepata taarifa kuwa mmoja wao tayari amepata maambukizi. Hata hivyo Dkt. Tulia hakumtaja jina mbunge huyo.

Dkt. Tulia alisema taarifa walizonazo ni kwamba mgonjwa huo anaendelea vizuri na Serikali inaendelea kumuangalia na kumpatia matibabu stahiki.

“Kwa maelezo ya mbunge huyo ni kwamba alisafiri kwenda Dar es Salaam siku za karibuni na aliporejea kuanzia Jumatano wiki iliyopita alianza kujisikia dalili kama ilivyotangazwa na wataalam wetu kuhusu virusi hivi vya corona.

Na baadaye akathibitishwa kwamba amepata maambukizi ya virusi hivi vya Corona,” alisema Dkt. Tulia.

Alisema Spika anawakumbusha na kuwasisitiza waendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na maambukizi ya corona kwa kufuata maelekezo ambayo wamekuwa wakipeana mara kwa mara.

“Pamoja na maelekezo hayo humu bungeni tumekuwa tukisisitizana kila wakati kwamba mbunge anayeingia bungeni ambaye ni zamu yake kuingia akae sehemu yake, asikae sehemu ya mbunge mwingine, akikaa sehemu ya mbunge mwingine tukianza kufuatilia nani alikaa karibu na nani, huyo

mbunge anayezunguka humu bungeni na kukaa kwenye viti vya wenzake atatupa wakati mgumu.

Kila mtu aone hili linamhusu yeye kama sehemu ya jamii, lakini pia kama kiongozi anayetamani kujilinda na kulinda watu wengine.”alisema Dkt. Tulia.

Aliwataka wabunge hao wajitaidi sana kukaa sehemu zao  ili wasitoe virusi sehemu moja kwenda sehemu nyingine na kwa kufanya hivyo watakuwa wamesaidia uongozi kujua huyo alikuwa anakaa hapa na changamoto imetokea hapa, hivyo wanaweza kuwafuatilia hao.

“Sasa ukiwa unazunguka kila sehemu na unakaa kila sehemu na unatumia kisemeo chochote unakuwa unatuweka sisi sote katika mazingira hatarishi na hata hizi hatua tunazozichukua itakuwa inatuwia ngumu sana kuendelea na huo utaratibu,” alisema.

Alisema wamekuwa wakijiwekea hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa wa Corona (COVID 19), lakini pamoja na jitihada hizo wamepata taarifa kuwa mmoja wao tayari amepata maambukizi.

Wakati huo huo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema sampuli zilizopimwa katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kati ya Aprili 18 hadi 20, mwaka huu zimethibisha kuwepo kwa wagonjwa wapya 87 wenye maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19) na kufanya idadi ya wagonjwa hao nchini kuwa ni 257.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana ilieleza kuwa kati wagonjwa hao, 16 walitolewa Taarifa na Waziri wa Afya wa Zanzibar jana Aprili 20, mwaka huu.

Kwa upande wa Tanzania bara wagonjwa walioongezeka na idadi yao kwenye mabano ni kama ifuatavyo; Dar es Salaam (33), Arusha (4), Mbeya (3), Kilimanjaro (3), Pwani (3), Tanga (3), Manyara (2), Tabora (1), Dodoma (3), Arusha (3), Ruvuma (2), Morogoro (2),Lindi (1), Mara (1), Mwanza (3),Mtwara (1),Kagera Rukwa (2).

Taarifa hiyo ilieleza kwamba wagonjwa wote walioripotiwa Tanzania Bara wanaendelea vizuri isipokuwa wagonjwa wanne wanaopatiwa huduma za wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum.

Aidha, Aprili 18, mwaka huu Waziri wa Afya wa Zanzibar alitoa Taarifa ya uwepo wa wagonjwa 23. Ongezeko la wagonjwa wapya linafanya idadi ya watu waliopata maambukizi ya ugonjwa wa Corona nchini kufikia 257 kutoka wagonjwa 147.

Aidha, Waziri Ummy alisema wanasikitika  kutangaza vifo vitatu vilivyotokea jijini Dar es Salaam vya watu waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya COVID-19.