April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbowe:Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu 2025 tutaweka wagombea kila nafasi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Freeman Mbowe, amesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025 utakuwa wa kufa na kupona kwakuwa wataweka wagombe kila nafasi itakayo tangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mbowe amesema hayo jijini hapa leo,Machi 8 2024 alipokuwa akitoa hotuba yake kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.

Amesema kwa kufanya hivyo hakuna mgombe yeyote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye atapita bila kupigwa kama ambavyo imekuwa katika miaka iliyopita.

Mbowe,amesema katika uchaguzi huo CHADEMA wamepanga kuwe mgombe kila nafasi itakayo tangazwa na NEC, katika ngazi zote kuanzia kitongoji hadi taifa.

“Uchaguzi ujao utakuwa wa kufa na kupona CHADEMA tutahakikisha tunaweka wagombea kila nafasi itakayo tangazwa lazima kila mgombe atakaye jitokeza CHADEMA tuwepo pale kumpinga hakuna kupita bila kupingwa”amesema Mbowe.

Alisema kutokana hali hiyo anamwagiza katibu mkuu wa Chama hicho pamoja na mfumo mzima wa chama kuhakikisha kuwa kila eneo anapatikana kipngozi bora na siyo bora kiongozi.

“Lazima mhakikishe kila eneo anapatikana mtu wa kwenda kugombea na awe na uwezo wa kushinda siyo kushiriki na kwa kiongozi yoyote ambaye atashindwa kuweka mgombea chama hatutamchekea katika hilo tutachekea kwa mambo mengine siyo hilo lazima tuwe na uchungu sisi ndiyo tutaweza kuondoa huu msiba wa CCM”amesisitiza Mbowe

Amesema CHADEMA ndiyo Chama pekee ambacho kitakwenda kumaliza malalamiko ya wananchi ambako hivi sasa wanalalamikia ugumu wa maisha.

Aidha, amesema wanachoomba ni Tume huru ya uchaguzi na katiba mpya kwani ndiyo itasaidia kumaliza tabia ya kuingia madarakani kwa viongozi ambao hawana kibali cha watu na Mungu.

“Asilimia 90 ya viongozi waliopo madarakani hivi sasa wengi wao wamengia katika nafasi hizo kwa njia zisizo za haki kutokana na uwepo wa tume hii ya uchaguzi hali ambayo imesababisha uwepo wa ufisadi,uminyaji haki na uvunjifu wa demokrasia nchini”amesema

Alisema hivi sasa wanachi wanalalamika gharama za maisha kupanda lakini wabunge ambao wamechaguliwa kuwawakilisha wananchi wanajiongozea mishahara.

“Mfumuko wa bei umepanda mara tatu lakini wabunge mwaka jana wamejipandishia mishahara hadi milioni 18 kwa mwezi”amesema Mbowe

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) Catherine  Ruge,amesema CHADEMA inapinga kitendo cha Bunge kupitisha sheria ya wenza wa viongozi kulipwa mafao huku kikishauri kufanyiwa kwa marejeo ya sheria ya Kikokotoo ambacho kimekuwa kikilalamikiwa na watumishi.

“Wananchi wengi bado wanakabiliwa na shida nyingi sana ikiwemo afya,huduma za maji, miundombinu na kupanda kwa gharama za maisha lakini leo bunge linapitisha sheria ya wenza wa viongozi kulipwa mafao.

“Wapo watumishi wa umma kwa mfano muuguzi wa ngazi ya cheti analipwa mafao ambayo hayaeleweki lakini leo hii Bunge linapisha sheria ya wenza wa viongozi kilipwa mafao”amesema Ruge

Amesema BAWACHA inashauri Bunge kufanya marejeo ya sheria ya kikokotoo ambayo yatawezesha kufanyika kwa maboresho ambayo yataleta ahuweni kwa watanzania wa hali ya chini.

“Bunge lipo kwa ajili ya kutetea wananchi wanyonge siyo watu watatu ambao ni wenza wa viongozi wanaotaka leo waume zao walipwe na wao walipwe pia”amesema