May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbowe apata chanjo ya COVID 19, CHADEMA yaomba kukutana Rais

CHADEMA yaikubali hotuba yake asema imegusa mioyo yao, Adai hawakusudii kumzengua, 

Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Dar es Salaam

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemuandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wakiomba kukutana kwa  maelezo kuwa hotuba yake ya kwanza aliyoitoa Machi 19, mwaka huu mara baada ya kuapishwa imegusa mioyo ya watu wengi wenye hofu ya Mungu wakiwemo wana-CHADEMA.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam leo na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe kupitia hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii.

Mbowe  amesema  pindi watakapokubaliwa kukutana na Rais Samia, hawakusudii kumzengua wala na wao hawatarajii kuzenguliwa, hasa kwa kuzingatia kwamba hotuba yake hiyo ya Machi 19, mwaka huu imegusa mioyo ya watu wengi wenye hofu ya Mungu, wakiwemo wana-CHADEMA.

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe

Mbowe alitumia fursa hiyo kunukuu baadhi ya maneno aliyoyasema Rais Samia kwenye hotuba yake, amesema;

“Katika kipindi hiki cha maombolezo huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu kama Taifa, kufarijiana, kuonesha undugu, sio wakati wa kuangalia  mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa kujiamini. Ni wakati wa kufutana machozi na kufajiriana “

Kwa mujibu wa Mbowe kutokana na kuguswa na maneno yake hayo, yeye kwa niaba ya CHADEMA tayari amemwandikia Rais Samia barua ya kuomba kukutana naye.

“Tumeomba rasmi kukutana naye ili tuweze kumueleza kilio chetu, hatutegemei  kumzengua, wala hatutegemea kuzenguliwa. Tunataka kumueleza tuliyonayo kwenye mioyo yetu na kumkabidhi mapendekezo ya kina kuhusiana na namna ya kujenga mtengamano wa taifa letu,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema kwa sasa wanatambua majukumu ya Kitaifa aliyonayo Rais  Samia, lakini wanatambua kuwa atawapa nafasi ya kuwasikiliza.

Ushindani wa kujenga

Aidha, Mbowe amesema wao kama CHADEMA wanamshauri Rais Samia kujiandaa kupata ushindani wenye kujenga sio wenye lengo la kubomoa.

“CHADEMA hatutaki visasi , bali  tunataka kushindana kwenye ushindani huru na wa haki,” amesema Rais Magufuli.

Asema TRA wamefungua kaunti zake

Katika hatua nyingine, Mbowe amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imemwandikia barua ya kufunguliwa akaunti zake zote zilizokuwa zimefungwa kwa madai ya kudaiwa kodi ya sh. bilioni mbili.

Amesema wakati wa akikabiliwa na kesi ya uchaguzi, Novemba 23, mwaka jana  yeye pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko walifutiwa dhamana baada ya kukiuka masharti ya dhamana..

Amesema akiwa gerezani Novemba 30, mwaka jana TRA walimwandikia barua    kumjulisha kuwa mojawapo ya kampuni yake ilikuwa inadaiwa kodi ya sh. Bilioni 2 , jambo alilodai halikuwa la kweli.

Amesema wakati TRA inamwandikia barua hiyo, alikuwa gerezani hivyo, hakuwa na namna ya kujibu TRA, japo alipewa siku 60 kama ana pingamizi.

Mbowe amesema baada ya siku 60, aliandikiwa barua ya pili na TRA, akijulishwa kwamba asipojibu ndani ya siku 30  itaonekana kwamba deni la kodi hiyo ni  halali, lakini hakuna namna ya kufanya hivyo kwa sababu alikuwa gerezani..

Kwa mujibu wa Mbowe, alivyotoka gerezani alizungumza na mamlaka zote husika, lakini  akaunti zote zilifungwa.

“Juzi nadhani baada ya hotuba ya Rais Samia katika mazingira ya kushangaza TRA wameniandikia barua kwamba wamefungua akaunti zangu, hawakunieleza kuhusu fedha zangu walizozichukua,” amesema Mbowe na kuongeza; 

“Hiyo ni moja ya sababu iliyonifanya niondoke nchini nikaamua kwenda nje kufanya biashara ya kimataifa,” amesema Mbowe.

Apata chanjo ya CORONA

Katika hatua nyingine, Mbowe aliweka wazi kuwa tayari amepata chanjo ya Corona katika nchi aliyokuwepo, lakini hakutaja ni nchi gani.

Aliunga mkono uamuzi uliotangazwa hivi karibuni na Rais Samia wa kuunda Kamati itakayomshauri kwenye masuala ya Corona.

“Binafsi naunga mkono mwelekeo uliooneshwa na Rais Samia katika suala zima la ugonjwa wa CORONA. Namuomba Mama Samia aunde haraka Kamati ya CORONA na hata pale ambapo hatuna wataalam wa kutosha, tuweze kupata wataalam kutoka nchi tofauti ili waweze kutushauri namna ya kuweza kukabiliana na jambo hilo,” amesema Mbowe.

Katiba Mpya

Akizungumzia madai ya Katiba mpya,  Mbowe amesema hilo; “Hitaji la Katiba mpya halitakiwi kuwa hitaji la Rais au chama chake. Uhitaji wa Katiba mpya hauhitaji kuwa utashi binafsi wa Rais  na chama chake kwani mjadala ulishafungwa,  hilo  ndilo  hitaji la Watanzania.”

“Hatupashwi kuwa na  mjadala wa kama  tunahitaji au hatuhitaji Katiba, mjadala unatakiwa  kuwa tunahitaji utaratibu gani kuweza kufikia huko,” amesema na kuongoza kwamba lazima tuwe na Katiba ambayo itaunda taasisi.