May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbaroni kwa tuhuma za kujiteka ili apewe milioni 5 na ndugu zake

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Zayoga John Juma(28) mfanyabiashara wa mbao mkazi wa Mkuyuni wilayani Nyamagana mkoani hapa kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa ili kujipatia kiasi cha milioni 5 fedha kwa ajili ya mtaji kutoka kwa ndugu zake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa baada ya mahojiano mtuhumiwa aliweka wazi kuhusu tukio hilo kwamba aliamua kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa ili aweze kupata fedha za mtaji wa biashara yake ya kuuza mbao ambazo alitarajia kuzipata kutoka kwa ndugu na
marafiki zake ambao wangemuonea huruma baada ya kueleza kuwa ametekwa na watu wasiojulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa Aprili 24,2024 Mutafungwa, ameeleza kuwa Aprili 9,2024 jeshi la Polisi mkoani hapa lilipokea taarifa kutoka kwa wakazi wa Mwanza ambao ni George Mapunda(34)mfanyabiashara na mkazi wa Iloganzala Pasiansi wilayani Ilemela na Veronica Zayoga(30), mkazi wa Sengerema walieleza kuwa ndugu yao aitwaye Zayoga John Juma,miaka ambaye ndiye mtuhumiwa huyo ametoweka na jitihada za kumtafuta hazijafanikiwa.

Ameeleza kuwa taarifa hiyo ilipokelewa kituo cha Polisi Nyamagana ambapo lilifunguliwa jalada la uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

Mutafungwa ameeleza kuwa baada ya taarifa hiyo jeshi hilo lilianza kufanya uchunguzi mara moja kuhusiana na kutoweka kwa mfanyabiashara huyo.

Pia ameeleza kuwa awali kabla ya tukio hilo Aprili 3,2024 majira ya saa 6 mchana
watoa taarifa hao George Mapunda na Veronica Zayoga walifika kituo cha Polisi Nyamagana wakiongozana na ndugu yao Zayoga
Juma ambaye alitoa taarifa kuwa amekuwa akifuatiliwa na watu wasiojulikana wakiwa na gari Toyota Land Cruiser rangi ya silver ambayo hakufanikiwa kutambua namba zake za usajili.

“Mara moja tulianza ufatiliaji na uchunguzi wa kina ili kubaini uhalisia wa
tukio hilo,wakati upelelezi kuhusiana na tukio hilo unaendelea Aprili 11,2024,tulifanikiwa kupata taarifa kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki wa Zayoga John Juma kuwa kwa muda tofauti amewapigia simu ndugu zake hao akawajulisha kuwa ametekwa na watekaji walimtaka kutoa kiasi cha shilingi milioni kumi ili wamwachie,”ameeleza Mutafungwa.

Pia aliwajulisha kuwa ili aweze kujinusuru kutoka mikononi mwa watekaji hao tayari
ameshawapa kiasi cha shilingi milioni tano alizozitoa kwenye akaunti yake ya benki
huku akiwaeleza kuwa hatoachiwa huru hadi akamilishe kiasi walichotaka watekaji hao.

Hivyo aliwaomba ndugu zake hao wamtumie fedha hiyo haraka kupitia namba yake ya
simu ili azitoe na kuwakabidhi watekaji.

Baada ya taarifa hizo Makachero wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza waliendelea na ufuatiliaji wa kina kuhusu tukio hilo huku wakishirikiana na taasisi nyingine za serikali kwa kufuatilia mienendo ya Zayoga John Juma tangu Aprili 3,2024 alipofika kituo cha Polisi
kuripoti kuwa anafuatiliwa na watu wasiojulikana wakiwa na gari Toyota Land Cruiser rangi ya silver ambalo hakuweza kuzitambua namba zake za usajili.

Mutafungwa ameeleza kuwa ilipofika Aprili
13,2024 majira ya 2 usiku jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo huko Tunduma Mkoa wa Songwe akiendelea na shughuli zake akiwa ni mwenye afya njema.

“Jeshi linatoka wito kwa watu wenye tabia kama hii iliooneshwa na kijana huyu kuwa halitawafumbia macho wote watakao husika kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo zinazoleta taharuki katika jamii,mtuhumiwa anashikiliwa kwa mahojiano zaidi na tayari ameshafikishwa hospitalini kwa uchunguzi wa kitabibu na atafikishwa mahakamani kwa kutoa taarifa za uongo,”.