March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mwa Afrika(SADC) ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Kanali.Wilbert Ibuge, Akizungumza katika Mkutano huo ambao unaowahusisha Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, Fedha na Mipango, Viwanda na Utalii kutoka SADC waliokuwa wakijadili kuhusu mwenendo wa Covid-19 kwa Nchi za SADC uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Tanzania

Mawaziri SADC, waridhia usafirishaji bidhaa muhimu, kudhibiti maambukizi ya Covid-19

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), limeridhia usafirishaji wa bidhaa muhimu katika ukanda  huo wakati wa janga la homa ya mapafu (Covid-19) ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa nchi wanachama.

Akizungumza katika Mkutano wa dharura wa Maafisa Waandamizi wa SADC, kuhusu Covid-19,  uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC na Waziri wa Mambo ya Nje kutoka Tanzania, Prof.Palamagamba kabudi alisema kuwa Baraza limepitisha mapendekezo ya Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya uliofanyika Machi 9, 2020, Dar es Salaam, Tanzania.

“Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya wa tarehe 9, Machi 2020, ulitoa mapendekezo ambayo yamefanyiwa kazi na Mkutano wa Baraza la Mawaziri yakiwa ni   ufuatiliaji na utekelezaji masuala ya afya kuhusu mlipuko wa Covid-19, kujadili namna ya kujiandaa na kukabiliana na virusi vya Covid -19,kubaini wagonjwa na kufuatilia waliokutana nao na huduma za tiba katika ukanda wetu” Alisema Prof. Kabudi.

Alisema masuala mengine ni uchunguzi na upimaji wa kimaabara, uzuiaji na udhibiti wa maambukizi, uelimishaji wa madhara na ushirikishaji wa jamii, uratibu wa kikanda wa kukabiliana na Covid-19, uwezeshaji na usafirishaji wa bidhaa muhimu katika ukanda huo wa SADC wakati huu wa Covid-19.

Mengine yaliyopitishwa ni Covid-19 na uwezeshaji wa biashara, Covid-19 na masuala ya udhibiti biashara na usimamizi wa majanga hatarishi katika ukanda huo wa Nchi za Kusini mwa Afrika, mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba  Covid-19 imeendelea kusambaa  duniani kwa hiyo Jumuiya ikaona iweke mikakati madhubuti kukabiliana na ugonjwa huo.

“Mkutano huu wa Baraza la Mawaziri SADC uliitishwa kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa maambukizi na vifo katika baadhi ya nchi Duniani, kwa mujibu wa taarifa namba 76 ya Shirika la Afya Duniani(WHO), ya April 5, 2020 inaeleza kuwa takribani watu 1,133,759 wameambukizwa ugonjwa huo na kati ya hao matukio mapya ni 82,061 na vifo 62,784 huku Afrika kwa nchi 51 kuna wagonjwa 9,198 na vifo viko chini ya watu 500, lakini kwa ukanda wetu wa SADC kuna matukio 2,127 katika nchi 14 huku vifo vikiwa 38” Alisema Prof.Kabudi.

Aidha, Prof. Kabudi alieleza kuwa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri uliofanyika sambamba na Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa SADC ulilenga katika kupokea taarifa ya wataalamu pamoja na muongozo wa urazinishaji na uwezeshaji usafirishaji wa bidhaa muhimu na huduma katika nchi za SADC wakati huu wa mlipuko wa Covid-19.

Bidhaa zilizopitishwa kwenye muongozo ni pamoja na usafirishaji wa vyakula, vifaa tiba, Dawa na vifaa vya kujinga na Corona, mafuta na mkaa wa mawe, pembejeo za kilimo na madawa, vifungashio, bidhaa zote zinazotumika katika utengenezaji, uchakataji na uhifadhi wa vyakula na vifaa ambavyo vinahusu usalama na dharura kwenye majanga mbalimbali.

Prof. Kabudi aliongeza kuwa SADC wamefanya hivyo ili kuzuia kuenea kwa Covid-19  na kuwezesha utekelezaji  mikakati ya kitaifa ya kupambana na ugonjwa huo na kuwezesha upatikana wa bidhaa muhimu ili kuzuia usafirishaji usio wa lazima kwa abirika katika ukanda huo wa Afrika .