April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matumizi ya tafiti za uwepo madini utavyopunguza uharibifu wa mazingira

Na Christopher Lilai,TimesMajira Online

KAZI ya utafiti wa uwepo wa madini katika eneo fulani ni hatua ya awali nay a muhimu sana katka uchimbaji wa madini.

Watu wengi nchini hawaoni umuhimu wa hatua hiyo wakati kimsingi ndiyo inayotoa taarifa za msingi zinazosaidia kazi ya uchimbaji kuwa ya ufanisi.

Lakini ili kuleta maana zaidi,ni muhimu kwa taarifa za utafiti kuwa wazi kwa wachimbaji wa madini. Hii itawasaidia wachimbaji hao kuelekeza nguvu za katika maeneo ambayo utafiti umeonyesha kuwa kuna madini ya kutosha na hivyo kupunguza uharibifu wa mazingira.

Chini ya utaratibu unaotumiwa na wachimbaji wengi hivi sasa, ikitokea tu fununu kuwa kuna madini katika aneo fulani, basi wachimbaji watavamia na kuanza kuchimba eneo lote wakati kukiwa na taarifa za utafiti zitanyesha madini yapo katika sehemu zipi.

Upo utafiti mwingi uliofanywa na wataalamu wa miamba kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini ambao umeleta taarifa kuhusiana na uwepo wa madini. Lakini kwa bahati mbaya taarifa hizo hazijawekwa wazi hasa kwa wachimbaji wadogo.

Badala yake wachimbaji hao hukimbilia maeneo ambayo mmoja wao amehabatika kupata madini mengi kwa mpigo wakiamini kuwa eneo hilo lote lina madini.

Kiufupi, wachimbaji wengi wadogo hufanya kazi hiyo kwa kugahatisha.

Matokeo yake,wachimbaji wanavamia eneo, wanachimba eneo lote na kufanya uharibifu wa mazingira wakati kimsingi eneo hilo halina madini mengi au halina madini kabisa.

Robert Makota, mchimbaji mdogo wa dhahabu katika machimbo ya Ikungu wilayani Nachingwea, mkoani Lindi,anabainisha kuwa kama taarifa za utafiti unaofanywa na wataalamu wa jiolojia zingewekwa wazi kwao kwa kubainisha eneo yalipo madini na kiasi kilichopo, kungepunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira unaotokana na wachimbaji ‘kuvamia’ kila aneo ambalo wanahisi kuwa kuna madini.

Anashauri kuwa baada ya eneo kugundulika kuwa lina madini ni vyema serikali kupitia wataalam wa miamba ikafanya utafiti wa kina ambao utabainisha na kutumbulisha maeneo mahsusi ambapo madini hayo yapo na kiasi kilichopo na yapo kwa kina gani.

Anasema taarifa hizo zitwasaidia wachimbaji kujikita katika maeneo yenye madini tu na kwa zana zinazofaa kuyafikia kwa urahisi na gharama nafuu.

Kwa msingi huo,maeneo karibu na maeneo yenye madini yatanusurika kuchimbwa bila sababu za msingi.

“Hali ilivyo hivi sasa inatisha utakuta eneo kubwa lina mashimo mashimo, miti imekatwa, hakuna huduma stahiki za kijamii kama vile vyoo na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Mpaka itakapofika wakati wachimbaji kubaini kuwa eneo hilo halina kitu, tayari eneo lote linakuwa limeshaharibiwa,” anafafanua Makota.

Akizungumzia eneo la Ikungu mathalani,anasema kuwa utafiti uliofanyika baada ya wachimbaji wadogo kupata dhahabu ulionyesha kuwa eneo hilo la Ikungu lina madini ya kutosha ndipo wakaaza uchimbaji.

Lakini kundi kubwa la wachimbaji, kwa tama ya kujipatia kipayto nao ‘wakavamia’ eneo hilo na kuchimba hata maeneo ambayo hayana madini.

“Awali hapa paligunduliwa na wachimbaji wadogo ambao walikuwa wanatafita madini kwa kubahatisha na kwa bahati wakapata madini kidogo.

“Serikali ilileta watafiti na baada ya utafiti tukaambiwa kuna madini mengi sana lakini hawajatuambia ni eneo gani hasa madini hayo yapo, matokeo yake sisi tunahangaika tu kuchimba kila sehemu hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira,” anasema Makota.

Kwa upande wake, Meneja wa Mgodi wa Mpiruka, ambao nao upo wilayani Nachingwea,Selemani Ngoso,alieleza kuwa waliingia kwenye mgodi huo mwezi wa sita mwaka 2020 baada ya kusikia kuna madini lakini bila kuwepo kwa utafiti wowote.

Kwa kuwa hawana taarifa kuhusiana na madini kayika eneo hilo, wachimbaji wamekuwa wakichimba eneo lolote wanalohisi kuwa wanaweza kupata chochote na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Meneja wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini, Jamal Baruti, alikiri kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na wachimbaji wadogo ambao wanavamia maeneo bila kufuata utaratibu hasa yanapogundulika madini.

Anabainisha kuwa taratibu na sheria inataka kabla wachimbaji hawajaanza kazi zao za uchimbaji ni lazima ufanyike tathimini ya athari ya mazingira katika eneo husika na yatolewe maelekezo ya namna gani uchimbaji unatakiwa kufanyika bila kuathiri mazingiza katika eneo husika.

Kutokana na wachimbaji wengi kufanya shughuli zao bila kujali tathimini ya athari kwa mazingira, anasema kuwa watalaamu kutoka ofisi yake wamekuwa wakitembelea maeneo hayo na kutoa elimu ya utunzaji mazingira.

“Tunatoa maelekezo ya nini wachimbaji wanapaswa kufanya ili kupunguza au kuondoa athari kwa mazingira. Tunawaelekezeza kama vile kufukia mashimo wakikamilisha kazi zao za uchimbaji na kupanda miti katika maeneo hayo kabla hawajaondoka na kuhamia eneo jingine.

“Tunafanya hivi kwa sababu wachimbaji wadogo ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira kwani wana tabia ya kuvamia maeneo ambayo yanajitokeza kuwa na madini bila kufuata utaratibu wa kisheri.”

Anaeleza kuwa iwapo itabainika wachimbaji wanafanya shughuli za uchimbaji bila kuwa na kibali cha NEMC uchimbaji huo unasimamishwa na hatua kali zinachukuliwa kwa anayemiliki mgodi