May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashirika ya Umma yasiyofanya vizuri kukiona

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

SERIKALI imesema Mashirika ya Umma yasiyofanya vizuri ndani ya miezi sita yatashughurikiwa ipasavyo ili kuleta tija kwa mustakabari mzima wa Taifa.

Lengo la kufanya hivyo, yanatakiwa kufanya kazi kwa ufanisi ili kuiletea faida serikali na pia kusonga mbele kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi.

Hayo yamesema leo na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na Wahariri wa Vyombo vya Habari.

Msechu amesema, umefika wakati Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma kufanya kazi kwa uweledi katika kuhakikisha wanapata mafanikio katika utendaji wao.

“Lengo ni kuhakikisha mashirika ya umma yanafanya kazi kwa ufanisi na kuleta faida kwa serikali katika kuhakikisha yanasonga mbele.

“Ili mashirika ya umma yapige hatua yanapaswa kutoingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake, kuwekeza rasilimali fedha katika kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuwekeana malengo na wasimamizi katika kufikia viwango vya mafanikio ndani ya muda fulani,” amesema Mchechu.

Amesema, mipango iliyopo kutakuwa na utaratibu wa kuishirikisha Mamlaka kwenye mchakato wa kuwapata wenyeviti, wajumbe wa Bodi na watendaji wakuu wa taasisi jambo ambalo itasaidia katika ufanisi wa kazi.

Aidha, amesema taasisi za umma zinapaswa kuwekewa mifumo rafiki ambayo itasaidia kutengeneza mapato na kuleta tija kwa Taifa.

“Ili kufikia malengo tumependekeza mambo muhimu ya kuzingatia ikiwemo kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (PIA), kwa kubadilisha jina la ofisi ya Msajili kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investment Authority- PIA) ili kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa duniani,” amesema.

Katika hatua nyngine, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji wa shilingi trillioni 73 katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala wa Serikali 298 ambazo zinafanya shughuli mbalimbali, huku asilimia 86 za taasisi hizo zikitoa huduma za kijamii.

Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu, amesema kutokana na mipango na mikakati iliyopo baada ya miaka mitano baadhi mashirika yanakwenda kufanya vizuri, huku watendaji wa mashirika hayo watapimwa kutokana ufanisi wa kazi katika kuhakikisha wanafikia malengo.

Mchechu amesema, kutokana uwekezaji huo kwa mwaka wa fedha 2022/23 mashirika 108 yameweza kupata mapato ya shilingi bilioni 777.

Amesema, kwa mwaka 2021/2022 mashirika 136 yameweza kupata mapato ya shilingi bilioni 645 na mwaka 2020/2021 mashirika 200 yamepata bilioni 477, huku mwaka 2019/2020 mashirika 236 yameingiza mapato ya bilioni 696.

Hata hivyo amesema, kuanzishwa kwa mfuko wa serikali kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati itasaidia kuongeza ufanisi wa uendeshaji, kuokoa mashiriki ambayo bila mfuko huo yanaweza kuanguka pamoja na kuwezesha mashirika ya umma kustahimili ushindani.

“Kuainisha vyanzo vya fedha za mfuko wa uwekezaji wa umma ambapo vyanzo vya fedha za mfuko vitakuwa ni pamoja na sehemu ya maduhuli yatakayokusanya na mamlaka ambayo kiwango chake kitabainishwa kwenye kanuni,” amesema Mchechu.

Nae Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deogratius Balile alitoa pongezi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuwfanya kazi kwa ufanisi huku akieleza kuwa vyombo vya habari vitaendelea kutoa ushirikiano katika masuala mbalimbali kuhusu serikali inavyopiga hatua.