May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Masauni ataja mafanikio Mambo ya Ndani mwaka mmoja wa Rais Samia

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

KATIKA kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefanikiwa katika kuimarika kwa hali ya Ulinzi na Usalama; kupandishwa vyeo kwa Maafisa, Wakaguzi na Askari; kukamilisha Malipo ya stahiki za Maafisa, Wakaguzi, Askari na watumishi Raia; kutoa ajira kwa askari wapya kukamilisha Malipo ya wazabuni na watoa huduma mbalimbali; kutoa Mafunzo kwa Maafisa, Wakaguzi na Askari kwa ajili ya upandishwaji vyeo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, aliyataja mafanikio mengine ambayo ni pamoja na Ujenzi wa Ofisi, Vituo vya Polisi na Nyumba za Makazi kwa Maafisa na askari wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyo chini ya Wizara hii, kutoa Nishani, kwa viongozi,maafisa naVyombo vya usalama.

Aidha, Waziri Masauni aliitaja Miradi mbalimbali ambayo imetekelezwa na Wizara hiyo;

“Miradi iliyotekelezwa ni pamoja na jeshi la Polisi, jeshi la magereza, idara ya uhamiaji, jeshi la zimamoto na uokoaji, makusanyo ya maduhuli,ajira kwa askari, mabadiliko ya sheria mbalimbali, usajili na utambuzi wa wananchi, kupambana na Biashara haramu ya usafirishiji wa binadamu, kupunguza msongamano wa wafungwa, kupunguza gharama na urekebishaji wa wafungwa , masuala ya huduma kwa wakimbizi na kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa na Kikanda katika kuzuia na kutanzua uhalifu nchini”

Mbali na hayo Waziri Masauni alisema Maafisa Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali walipata mafunzo ambayo yamewaongezea uwezo wa kiutendaji na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Vyombo hivyo;

“Jumla ya Maafisa Wakaguzi na Askari 34,000, wamehudhuria mafunzo ya kada mbalimbali kulingana na nafasi zao ambapo Jeshi la Polisi, Maafisa Wakaguzi na Askari 24,285 wamehudhuria mafunzo husika, Jeshi la Magereza, Maafisa Wakaguzi na Askari wamehudhuria mafunzo husika, 8,181, Idara ya Uhamiaji, Maafisa Wakaguzi na Askari wamehudhuria mafunzo husika ambapo Maafisa 336 na Askari 344 Jumla yao ni 780 na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Maafisa Wakaguzi na Askari wamehudhuria mafunzo husika, 918.”

Aidha Waziri Masauni alisema Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, jumla ya Maafisa, Wakaguzi, Askari na Watumishi raia 34,698 wamepandishwa vyeo, ambapo kati yao; 34,106 ni Maafisa, Wakaguzi na Askari na 592 ni Watumishi raia ambao walistahili kupandishwa vyeo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019, 2019/2020 na 2020/2021

Kuhusu NIDA Masauni alisema Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanikiwa kusajili wananchi 1,061,998 katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, hivyo kufanya jumla ya Wananchi 22,881,902 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo.

Mbali na hayo Waziri Masauni alisema Wizara kupitia Sekretarieti ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wadau 280 wanaohusika na utekelezaji wa Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu.

Waziri Masauni alimaliza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaSamia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo ameiwezesha Wizara hiyo na taasisi zake zote ikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyoko chini ya Wizara hii, kupata mafanikio makubwa tangu alipoingia Madarakani.