April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mantra yatoa msaada wa gari, kisima cha maji kwa Hospitali ya Wilaya Namtumbo

Na Cresensia Kapinga,TimesMajira,Online Songea.

KAMPUNI ya Mantra Tanzania imetoa msaada wa gari aina ya Canter yenye thamani ya sh. milioni 50 na kisima kimoja cha maji chenye thamani ya sh.milioni 29 kwa Hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Msaada huo umetolewa jana na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Mantra Tanzania, Frederick Kibodya kwa hospitali hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Dkt.Julias Ningu.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Namtumbo.

Amesema msaada huo utasaidia jamii ya wakazi wa Wilaya ya Namtumbo na maeneo mengine.Kwa upande wa gari, alisema litasaidia kwa kiasi kikubwa kusambaza dawa na vifaa tiba kwenye vituo vya afya na zahanati zilizopo vijijini.

Amesema msaada huo unazidi kuwapa fursa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo na kuona ni namna gani wanaweza kukabiliana na changamoto zinazoweza kuwakabili na si vinginevyo.

“Sisi kama Mantra ni sehemu ya jamii ya wananchi wa Namtumbo, hivyo tunavyosaidia hospitali hii ni kwa manufaa ya wote maana hata sisi tunaweza kuja kutibiwa hapa kutoka Mkuju ambako shughuli za uchimbaji wa madini ya URANUM zinatarajiwa kuanza hapo baadaye,” amesema Kibodya.

Kibodya amefafanua kuwa kisima hicho ambacho kina uwezo wa kuhifadhi maji lita 10,000 kitawasaidia wagonjwa wanaofika kupata huduma hospitalini hapo pamoja madaktari na wauguzi.

Gari aina ya Canter lenye thamani ya sh. milioni 50 ambalo imekabidhiwa kwa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo na Kampuni ya Mantra Tanzania kwa ajili ya kubebea dawa na vifaa tiba. Kampuni hiyo inayojishughulisha na uchimbaji wa madini aina ya Uranium. Picha na Cresensia Kapinga.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Ningu baada ya kukabidhiwa msaada huo amesema Mantra imekuwa ikichangia shughuli mbalimbali za maendeleo katika Wilaya hiyo.

Amepongeza jitihada zinazoendelea kutolewa na Mantra na amewaomba wawekezaji wengine watajitokeza Wilayani humo na waige mfano wa kampuni hiyo ya Mantra.

Ameeleza zaidi kuwa miundombinu ya maji (kisima) pamoja na gari inapaswa kutunzwa ili msaada huo uwe ni endelevu na wa faida kwa jamii ya wanainchi wa Namtumbo na kwamba atakayebainika kuhujumu miradi hiyo serikali itashughulika naye.

Naye Munge wa Jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa amepongeza kampuni hiyo kwa kuendelea kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Namtumbo katika shughuli mbalimbali za maendeleo hasa pale inapotokea maafa.