April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BREAKING NEWS;Mama adaiwa kumuua mwanae wa miaka saba kwa kumchinja

Na Doreen Aloyce,TimesMajira, Online Dodoma

MTOTO wa miaka saba (Willy Wiliam) mwanafunzi wa dasara la tatu Shule ya Msingi Ihumwa ameuawa kwa kuchinjwa shingo na mtu anayedaiwa kuwa ni mama yake mzazi, Grace William (45) kisha kutokomea kusikojulikana.

Tukio hilo limetokea usiku wa manane kuamkia jana katika Mtaa wa Ihumwa, nje kidogo ya Jiji la Dodoma ambako mtoto alikuwa akiishi na mama huyo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ihumwa ambaye pia ni baba mzazi wa Grace, William Ngilimunji, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kwamba aliyekufa ni mjukuu wake. Alidai wakati mauaji hayo yanafanyika mtoto alikuwa amelala.

Amedai kwamba aliyehusika na mauaji hayo ni mama wa mtoto huyo ambaye ana matatizo ya akili na kwamba alikuwa akihudhuria kliniki Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Mirembe, mkoani hapa.

Ngilimunji amesema mtoto wake huyo (mama wa marehemu) hana mume na amekuwa akiishi Ihumwa. Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Mroto, alisema yupo nje ya mji na kwamba hajapata taarifa yoyote na aliahidi akirudi mjini atawataarifu waandishi wa habari.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya Polisi vimethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kwamba tayari mwili wa marehemu ulikuwa umechukuliwa na kuhifadhiwa chumba cha maiti Hospitali ya Mkoa Dodoma kwa ajili ya uchunguzi na taratibu za mazishi.