July 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makinda apongeza jitihada za Serikali kuhamasisha Nishati Safi ya Kupikia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisema zinaonyesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha matumizi ya mapishi safi nchini.

Makinda ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea maonesho ya teknolojia mbalimbali za nishati safi, ambapo alisema amevutiwa na ubunifu unaolenga kupunguza matumizi ya kuni, mkaa na nishati nyingine za jadi ambazo zimekuwa na athari kwa afya na mazingira.

Amesema matumizi ya vifaa vinavyookoa umeme na kutumia nishati safi ni hatua muhimu katika safari ya kuhamia kwenye matumizi ya nishati endelevu nchini.

“Hii ni hatua kubwa sana kuelekea matumizi ya nishati safi. Kampeni ya Rais Samia kuhusu mapishi safi inaendelea kuleta mwamko mkubwa na naamini mafanikio yake yataongezeka zaidi kadri wananchi watakavyoendelea kuelimishwa,” amesema.

Makinda amebainisha kuwa baadhi ya teknolojia zilizooneshwa zinafaa zaidi kwa mazingira ya vijijini kutokana na urahisi wa upatikanaji na matumizi yake, tofauti na baadhi ya teknolojia ambazo zinahitaji miundombinu zaidi.

Amesema pamoja na gesi kuwa suluhisho muhimu kwa maeneo mengi ya mijini, bado kuna changamoto ya upatikanaji wake katika baadhi ya maeneo ya vijijini, hivyo ni muhimu kuendelea kuwekeza katika teknolojia mbadala zinazokidhi mahitaji ya wananchi wa maeneo hayo.

Aidha, ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi yana faida kubwa katika kuboresha afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuongeza tija kwa wanawake kwa kuwaondolea mzigo wa kutafuta kuni na kutumia muda mwingi jikoni.

“Teknolojia hizi zinawapa wanawake nafasi ya kutumia muda wao katika shughuli nyingine za maendeleo na uzalishaji mali badala ya kutumia muda mwingi kutafuta kuni na kupika kwa njia za jadi,” amesema.

Makinda pia amewataka wadau wa nishati safi kuendelea kuandaa maonesho ya vitendo kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu faida za teknolojia hizo.

Amesema wananchi wengi huamini na kuelewa zaidi wanapoona matumizi ya teknolojia hizo kwa vitendo kuliko kusikia maelezo pekee katika mikutano.

Akihitimisha, amewapongeza waandaaji wa maonesho hayo pamoja na wanawake wanaoshiriki kuonesha teknolojia mbalimbali za nishati safi, akisema juhudi hizo zina mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kutumia nishati salama na rafiki kwa mazingira.