January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majibu ya papai kukutwa na Corona, ‘yatumbua’ vigogo

Na Penina Malundo

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amemtaka Katiba Mkuu (Afya) kuwasimamisha kazi mara moja Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii Dkt. Nyambura Moremi na Meneja Udhibiti wa Ubora Jacob Lusekelo ili kupisha uchunguzi.

Waziri ummy ametaka hatua hizo kuchukuliwa kufuatia hotuba ya Rais John Pombe Magufuli wakati akimuapisha Waziri wa Katiba na Sheria, kubainisha changamoto za utendaji wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.

Kufuatia changamoro hizo tayari Waziri ameunda kamati ya wataalam wabobezi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa Maabara ya Taifa ya Afya ya ikiwemo Mfumo mzima wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za COVID-19.

Kamati hiyo itaongozwa na Prof. Eligius Lyarnuya kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na wajumbe tisa ambao ni Prof. Said Aboud – Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (MUHAS), Prof. Gabriel Shirima – Chuo Kikuu cha Nelson Mandela (NMIST) na Prof. Steven Mshana – Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Buganda (CUHAS).

Wengine ni Prof. Rudovick Kazwala – Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Dkt. Thomas Marandu – Chuo Kikuu cha Data es Salaam (UDSM), Dkt. Mabula Kasubi -Hospitala Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Danstan Hipolite – Mamlaka ya Dawa Na Vifaa Tiba (TMDA), Viola Msangi – Mtaalam wa Maabara Mstaafu na Jaffer Sufi – Mtaalam wa Maabara Mstaafu.

Kamati hiyo itaanza kazi mara moja na itatakiwa kuwasilisha taarifa yao kwaWaziri kabla ya Mei 13, 2020 ambapo sambamba na uchunguzi wa kamati hiyo, shughuli za upimaji wa sampuli katika maabara zinaendelea.