May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa:Kukamilika kwa Hospitali ya Rufaa Songwe kutachochea Utalii wa matibabu

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Mbozi. 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Songwe ili kuimarisha huduma za afya zikiwemo za kibingwa na kwamba itakapokamilika itachochea utalii wa tiba kwa wagonjwa kutoka mataifa jirani ya Zambia na Malawi.

Amebainisha hayo leo Novemba 23, 2023 mara baada ya kukagua na kuridhisha na huduma zinazotolewa, ikiwemo maendeleo ya ujenzi wa baadhi ya majengo yanayoendelea kujengwa katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe iliyopo eneo la Hasamba, Wilayani Mbozi, kabla ya kuweka jiwe la Msingi, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu Mkoani hapa.

Waziri Mkuu amesema kuimarishwa kwa huduma za matibabu katika hospitali hiyo ambayo tayari imeanza kutoa huduma za kibingwa katika maeneo manne kutavutia wagonjwa kutoka mataifa hayo jirani ya Malawi na Zambia kuja kupata huduma katika Hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Songwe.

“Hospitali hii inajengwa hapa Songwe ni ya kimkakati kwani mkoa huu umepakana na nchi jirani za Zambia, lakini pia Malawi pale Ileje,

“Ndugu zetu hawa wa Malawi na Zambia kwa karibuni  hawana  huduma kubwa za kimatibabu kama zitakazotolewa hapa, maana yake ni nini wao watakuja hapa Mbozi kutibiwa kwa hiyo hapa tuna utalii wa matibabu,”amesisitiza Waziri Mkuu.

Awali akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu,  Mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya Rufaa Songwe (MOI),Dkt Juma Ramadhan Juma, amesema hadi kufikia sasa ujenzi wa hospitali hiyo umetumia zaidi ya sh. bilioni16,  ambapo kiasi cha sh.bilioni 13 zimetumika kwa ajili ya  ujenzi, hulu sh. bilioni 3.289 zimetumika katika  unuuzi wa vifaa tiba.

Dkt Juma aliongeza kuwa,hospitali  hiyo imeanza kutoa huduma za kibingwa katika maeneo makuu manne,ambayo ni huduma za kibingwa za  macho,magonjwa ya wanawake na afya ya uzazi, huduma bingwa za magonjwa ya watoto pamoja na huduma ya  dharura na ajali.

Aidha ,Dkt Juma amesema kuwa katika kipindi cha julai 2022 hadi juni 2023 hospitali hiyo imehudumia jumla ya wagonjwa 19,265 kati ya hao wagonjwa wa nje (OPD)17,929 na waliolazwa (IPD) ni 1336 kati ya hao kuna akina mama 695 waliojifungua salama hivyo kupunguza video vya akina mama vitokanavyo na uzazi na kufikia vitano (5).

Wakati huo huo,  Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amemueleza Waziri Mkuu kuwa ndani ya siku 21 wizara ya afya itakuwa imefunga mashine ya CT scan na mashine ya kisasa ya mionzi (digital x-ray) ambayo mfumo wake umeunganishwa na hospitali kubwa zote nchini ambapo mgonjwa ataendelea kupata huduma za kibingwa akiwa Songwe.