May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA: 2024 vijiji vyote kupatiwa umeme Tanzania nzima

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), imesema ifikapo Juni 2024, vijiji vyote hapa nchini, vitakuwa vimepatiwa umeme kutokana na mikakati waliojiwekea kuhakikisha hadhma hiyo inatimia

Hayo yalisema leo jijini Dar es Salaam, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa (REA), Mhandisi Jones Olotu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Hassan Saidy katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari hapa nchini, chini ya uratibu wa Ofisi ya msajili wa Hazina (TR).

Akizungumzia hilo, Mhandisi Olotu amesema Tanzania Bara kuna takribani vijiji 12,318, hadi kufikia jana vijiji 11,313 tayari vimeshaunganishiwa umeme, huku vijiji 1,005 bado lakini wakandarasi wapo kazini kuhakikisha navyo vinapatiwa umeme.

Amesema, wakandarasi wapo kazini kwa kasi kubwa, hivyo ifikapo mwezi wa sita mwakani REA, itakuwa imekamilisha vijiji vyote Tanzania nzima kuwa na umeme.

“Kutokana na kasi tulionayo na malengo tuliojiwekea, ifikapo mwezi wa sita 2024, tuna uhakika vijiji vyote vitakuwa vimeunganishwa umeme Tanzania nzima.

“Hii inatokana na sapoti kubwa tunayopata kutoka Serikalini pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo,” amesema Mhandisi Olotu.

Hata hivyo amesema, kutokana na muundo wa nchi yetu imeanza na Mikoa, Wilaya, Tarafa, Kata, vijiji, kwa hiyo mikoa na wilaya tayari umeme umeshaunganishwa kilichobaki kwenye vijiji, tarafa na vitongoji.

Olotu amesema, vitongoji vilivyopo nchini ni 64,760 kati ya hivyo 28,659 tayari vimeunganishwa umeme.

Mbali na hivyo, Mhandisi Olotu amesema mwaka 20230 malengo yao ni kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinapatiwa umeme.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Olotu alitaja changamoto zinazowakabili ikiwemo miundombinu kama vile Barabara, uharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji moto misitu ambayo upelekea kuungua kwa nguzo za umeme.

Ametoa wito kwa jamii kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kulinda miundombunu ya Nishati ili iweze kunufaika na vijiji viweze kupata umeme kwa wakati.

REA, ni tasisi ya serikali inayojitegemea ambayo ipo chini ya Wizara na Nishati, ikiwa na jukumu kubwa la kuhamasisha, kuratibu na kuwezesha uanzishwaji na uendelezaji wa miradi ya Nishati vijini.

Wakala wa Nishati Vijini (REA), ilianzishwa kwa Sheria ya Nishati Vijijini Na.8 ya mwaka 2005 na kuanza kazi rasmi mwezi Oktoba 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa iliyokuwa Sera ya Nishati ya mwaka 2003.