May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Tumieni kampeni msaada wa kisheria ya Mama Samia kutokomeza ukatili

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watanzania kuitumia kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutoa taarifa kuhusu uwepo wa watu, au vikundi vya watu ambao ama wanajihusisha na ukatili wa kijinsia hususan kwa watoto.

Ametoa wito huo leo Alhamisi (Aprili 27, 2023) alipozindua kampeni hiyo ambayo itatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia Machi, 2023 hadi Desemba 2025.

Amesema kuwa kampeni hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji haki, mifumo ya utoaji haki, masuala ya kisheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na taasisi za serikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika utoaji huduma kwa wananchi.

“Kampeni hii pia  itasaidia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa”. Amesema

Ameongeza kuwa, faida nyingine ya kampeni hiyo ni kusaidia kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi zote yaani kuanzia Serikali kuu hadi Serikali za Mitaa. “Ushiriki wa wadau wanaojihusisha na huduma ya msaada wa kisheria utaongezeka kwa asilimia 80 katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria iweke mfumo mzuri wa kushughulikia changamoto za kisheria zitakazoibuliwa wakati wa Kampeni katika utimilifu wake. “Tusiache wananchi wakiwa bado hawajapata majibu ya changamoto zao. Hii itasaidia kujenga taswira nzuri kwa Serikali wala kwa mamlaka ambayo imeridhia kuwepo kwa Kampeni hii”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara hiyo itekeleze majukumu yake kwa ufanisi na weledi mkubwa ili Watanzania wote waweze kuifikia haki na kuipata haki  kwa wakati.

“Kwa wale ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili wa kujitegemea hakikisheni wanapata huduma za kisheria bila ya upendeleo wowote na kwa viwango stahiki”.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa kampeni hiyo ambayo ni  maagizo ya Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanatoa elimu ya sheria na kusaidia wahitaji ndani ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, wamepanga kutoa elimu katika maeneo ya migogoro ya Ardhi, mirathi, ndoa, sheria ya mtoto katika maeneo ya Ukatili  wa kijinsia na Maadili

Amesema kuwa kampeni hiyo itatekelezwa pande zote mbili za Muungano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Serikali na wasio wa serikali ikiwemo Ofisi ya Mashtaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ustawi wa Jamii, vyuo vya elimu ya juu,

Wengine ni CHAMA cha Wanasheria nchini (TLS), Mtandao wa Mashirika yanayotoa huduma ya msaada wa kisheria – (TANLAP), Taasisi ya Huduma za Kisheria (LSF), LHRC, EU, UNDP, WILDAF na Benki ya NMB .

LSF kama mdau mkubwa wa upatikanaji wa haki imeshiriki Uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya Mama Samia Legal Aid. LSF inatoa ruzuku kwa mashirika ya wasaidizi wa kisheria 184 Tanzania Bara na Zanzibar na inawezesha watoa huduma za msaada wa kisheria zaidi ya 4500 kutoa huduma za msaada bure kwa wananchi. Pichani (watatu kulia waliosimama wakiwa wamevaa T-shirt) ni Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala katika picha ya pamoja na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa wakati wa uzinduzi wa ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’ uliofanyika 27.04.2023 Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa katika banda la LSF baada ya kutembelea ambapo alipata maelezo kutoka kwa Msaidizi wa Kisheria Mkoa wa Dodoma, Kapesa Mawazo, kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’ ulioanza 28 Aprili 2023 katika wilaya na halmashauri nane zikiwemo Mpwapwa, Kondoa, Bahi, Dodoma DC,
Chamwino, Chemba, Dodoma Mjini na Kongwa. Wasadizi wa kisheria ndio watekelezaji wa kampeni hii muhimu katika ngazi za wilaya hapa nchini wakishirikiana na wadau wengine.
Katika uzinduzi wa kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mkoani Dodoma leo, Waziri Mkuu nchini, Kassim Majaliwa Majaliwa alipotembelea banda la LSF na kuelezwa kazi zinazofanywa kupitia wasaidizi wa kisheria nchi nzima ikiwemo utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.
Pichani ni Meneja Rasilimali na Mawasiliano wa Legal Services Facility, Jane Matinde (mwenye shati jeupe) akifafanua jambo mbele ya Waziri Mkuu wa Tanzania wakati wa uzinduzi wa ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’ Jijini Dodoma uliofanyika 27.04.2023
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza na Wasaidizi wa kisheria kutoka wilaya ya zote za mkoa wa Dodoma mara baada ya kutembelea banda la LSF wakati wa tukio la uzinduzi wa ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’ kwenye Mkoa wa Dodoma uliofanyika 27.04.2023