March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akihotubia mkutano wa kampeni.

Majaliwa: Shule 28 Bariadi zanufaika na EP4R

Na Mwandishi Maalum, timesmajira, online Bariadi

SHULE 28 za wilaya ya Bariadi zikiwemo 11 za msingi na 17 za sekondari zimenufaika na mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa Lipa Kutokana na Matokeo (EP4R) uliotekelezwa tangu 2015 hadi 2020.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nkololo, wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nkololo ‘A’.

Akielezea utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wakazi hao, Majaliwa amesema awali zilitolewa sh. bilioni 2.3 na Septemba, mwaka huu zimetolewa sh. milioni 457 ili kukamilisha uwekaji miundombinu ya nyumba za walimu, madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi za Halawa, Kilabela A, Tunge, Mwauchumu, Bukiliguu, Byuna, Chungu cha bawawa, Damidami, Masewa C, Mwashagata na Banemhi zilizoko wilayani humo.

Wanawake wakionesha ishara ya kumpa kura za NDIYO mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais John Magufuli.

“Kwa upande wa shule za sekondari, sh. bilioni 1.07 zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya nyumba za walimu, madarasa, maabara, majengo ya utawala na matundu ya vyoo kwa sekondari za Dutwa, Mwantimba, Gegedi, Miswaki, Mwamlapa, Nkololo, Nyasosi, Nyawa, Sapiwi, Banemhi, Gasuma, Igaganulwa, Ikinabushu, Itubukilo, Mwadobana, Sakwe na Nkindwabiye.”

Kuhusu mpango wa elimu bila malipo, Majaliwa amesema shule za msingi 79 zilipatiwa shilingi bilioni 3.12 kwa ajili ya ukarabati wa majengo, masuala ya utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

Amesema shule za sekondari 23 zilipatiwa shilingi bilioni 1.43 kwa ajili ya kulipia fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.

Akielezea miradi ya barabara, Majaliwa amesema sh. bilioni 3.2 zimetolewa kupitia TARURA kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi, na ujenzi wa barabara zenye urefu wa km. 246 ambazo zimefanyiwa matengenezo kwa kiwango cha udongo, km. 37.6 kwa kiwango cha molamu. Pia, makalvati 108 yamejengwa.

Amezitaja barabara zilizofanyiwa matengenezo hayo kuwa ni za Ikungulyabashashi – Ditima; Byuna – Nkindwabiye – Halawa; Igegu – Matongo Gibishi – Halawa; Dutwa- Gilya – Mwauchumu; Nyakabindi – Mwadobana – Gasuma; Kasori Centre – Kasori Ginnery na Nyamswa – Mwasubuya – Bwawani.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi, Injinia Kundo Mathew, mgombea udiwani wa kata ya Nkololo, Nyamwela Sinda na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Bariadi waliokuwepo kwenye mkutano huo.