May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe kabla ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa bandari ya Kasanga wilayani Kalambo. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Majaliwa: Serikali itaendelea kudhibiti matumizi fedha za umma

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Kalambo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Pombe Magufuli itaendelea kudhibiti matumizi ya fedha za umma ili iweze kuendelea na ujenzi wa miradi ya kimkakati zikiwemo bandari kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi wake.

Pia, Waziri Mkuu amesema changamoto ya usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itakuwa historia baada ya kuboreshwa na kujengwa kwa miundombinu ya bandari katika wa Ziwa Tanganyika ukiwemo upanuzi wa bandari ya Kasanga.

Waziri Mkuu ameyasema hayo alipozungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa Bandari ya Kasanga iliyoko Wilaya ya Kalambo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Rukwa. Mradi huo unagharimu zaidi ya sh. bilioni 4.7.

Amesema upanuzi wa bandari hiyo utawezesha mizigo inayotoka nchini kwenda Congo kufika kwa wakati kwa sababu itasafirishwa moja kwa moja bila kupitia katika nchi nyingine kama ilivyo sasa, ambapo madereva wanalazimika kupita kwenye Mataifa mengine na kutumia muda mrefu.

“Mradi huu ukikamilika utaongeza pato la mwananchi mmoja mmoja pamoja na Taifa kwa ujumla. Rais Dkt. Magufuli amedhamiria kuboresha maendeleo ya wananchi nchi nzima ikiwemo na wilaya hii ya Kalambo. Ujenzi wa miradi hii unatoa fursa za ajira kwa wananchi, hivyo zichangamkieni.”

Vilevile, Waziri Mkuu amesema, mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa bado yanaendelea nchini, hivyo mtu yeyote atakayebainika anajihusisha na masuala hayo atafutwe popote alipo akamatwe na achukuliwe hatua za kisheria kwa sababu rushwa ni adui wa haki.

Pia, Waziri Mkuu ameendelea kuwakumbusha watendaji ndani ya Serikali wahakikishe wananchi wanapofika katika maeneo yao ya kazi wawapokee, wawasikilize na kuwahudumia bila ya ubaguzi. “Hatuangalii sura wala kabila yeyote atakayekanyaga kwenye maeneo yenu ahudumiwe ipasavyo.”

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alisema Tanzania na Congo zimeungana kwa Ziwa Tanganyika, usafiri wa barabara uliokuwa unatumika awali uliyalazimu maroli ya mizigo kupitia nchini nyingine na kuchelewa kufika.

Amesema, kukamilika kwa upanuzi wa bandari hiyo pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwago cha lami kutoka Sumbawanga hadi Kasanga kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kutumia bandari hiyo kuingia nchini Congo moja kwa moja bila kupita kwenye nchi juirani.