May 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahakama Kuu yazuia wasikilizaji rufaa ya Mbowe, vigogo CHADEMA

Mwenyekiti wa CHADENA, Freeman Mbowe

Na Grace Gurisha

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imesema hakuna mtu yeyote (wafuasi, mashabiki) atakayeruhusiwa kuingia mahakamani hapo kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mwenyekiti wa CHADENA, Freeman Mbowe na wenzake saba kupinga hukumu ya kifungo cha miezi mitano iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hivi karibuni.

Amri hiyo, imetolewa leo na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Lameck Mlacha, wakati rufaa hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa. Hatua huyo inalenga kuepuka mkusanyiko katika kipindi hiki ambacho nchi ipo kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa Corona.

“Siku ya usikilizwaji wa kesi wanaotakiwa kuwepo ni warufani wenyewe nane, mawakili wao na mawakili wa upande wa wajibu rufani”, amesema Jaji Mlacha.

Hata hivyo, Jaji Mlacha alipanga kesi hiyo kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Elvin Mgeta Mei 13, mwaka huu.

Katika rufaa hiyo namba 76 ya mwaka 2020 wakata rufani mbali ya Mbowe, wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya.