April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais John Magufuli

Magufuli, Rais wa Msumbiji wafanya mazungumzo kwa simu

Na Mwandishi Wetu

RAIS John Magufuli jana amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Msumbuji, Filipe Jasinto Nyusi ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala mbalimbali yahusuyo uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Msumbiji na masuala ya kikanda.

Rais Magufuli amempongeza na kumtakia heri Rais Nyusi na wananchi wote wa Msumbiji kwa Taifa hilo kuadhimisha miaka 45 ya tangu kupata uhuru wake.

Rais Magufuli amemwambia Rais Nyusi kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri wa kidugu, kirafiki na ujirani mwema na Msumbiji kama ulivyoasisiwa na Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Moses Machel wa Msumbiji katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, viongozi hao wamezungumzia maandalizi ya kupokezana kijiti cha uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa SADC atamkabidhi uenyekiti wa SADC, Rais Nyusi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa SADC kwa sasa.

Viongozi hao pia wamezungumzia ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) ambapo wamebadilishana mawazo juu ya namna bora ya kukabiliana na ugonjwa huo, hasa namna Tanzania ilivyofanikiwa kupunguza maambukizi yake.