Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar
MADIWANI wa Halmashauri ya Bukoba Vijijini (CCM), wamepongeza Serikali kwa kazi kubwa ya ujenzi wa miundombinu na kushauri kasi hiyo iendeleee kwenye miradi yote ya kimkakati.
Pia madiwani hao wameipongeza Serikali ya awamu ya tano na ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyotekeleza miradi hiyo kwa vitendo
Wameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam walipotembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Terminal III, Daraja la Mfugale, Daraja la Nyerere Kigamboni, Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la Tanzanite
Madiwani hao walikuwa jijini Dar es Salaam kwa ziara ya mafunzo kwa mwaliko wa Mbunge wa Jimbo hilo, Dkt. Jasson Rweikiza, ambapo pia walitembelea miradi mbalimbali mkoani Dodoma kabla ya kuja Dar es Salaam
Kwenye ziara hiyo wameambatana na Sekretarieti ya CCM Wilaya Wilaya ya Bukoba Vijijini na Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Diwani wa Kata ya Kanyangereko, Joasi Rweikiza amesema wamejionea wenyewe utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati kama Serikali ilivyoahidi.
“Tulikuwa tunasikia tu lakini kwa ziara hii tumejionea wenyewe na tunakwenda kuwaambia wananchi kwamba Serikali ya CCM inatekeleza Ilani ya chama kwa vitendo waendelee kuiunga mkono,” amesema
Alisema madiwani wenzake wamefurahishwa mno na kuona uwanja wa ndege mpya kwa namna ulivyojengwa kwa kwa viwango vya kimataifa
Amesema ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Mbezi kuelekea Kibaha Mkoa wa Pwani imeondoa tatizo la foleni ambalo lilisumbua kwa muda mrefu.
Amesema watu walikuwa wakitumia muda mrefu kutoka jijini Dar es Salaam kufika Kibaha lakini ujenzi wa barabara hizo umepunguza muda na kwa sasa dakika 20 tu zinatosha kufika Kibaha
Diwani wa Kata ya Buterankunzi, Gospel Mashongole, alisema wamejifunza kwa vitendo mambo mengi ambayo awali walikuwa wakiyasikia tu kwenye vyombo vya habari.
“Mfano ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar mpaka Mwanza tulikuwa hatujawahi kuona lakini leo tumeona wenyewe sasa tunawaambia watu waliokuwa wanabeza kwamba mambo yanafanyika kwa vitendo,” amesema
Amemshukuru Mbunge wa Bukoba Vijijini, (CCM), Dk. Jasson Rweikiza kwa ziara hiyo ya mafunzo ambayo alisema imewafumbua macho madiwani hao kwani awali hawakuwahi kujionea wenyewe utekelezaji wa miradi hiyo
Naye Dkt. Rweikiza amesema dhumuni la ziara hiyo ni kujifunza na walianzia Dodoma ambapo walijifunza mambo mbalimbali yanayofanywa na Bunge.
Amesema madiwani hao wamejionea wenyewe utekelezaji mkubwa wa miradi mbalimbali na wameahidi kwenda kuwaeleza wananchi kwamba serikali waliyoiweka madarakani inatekeleza ahadi zake kwa vitendo
“Miezi mitatu iliyopita kuna Sh bilioni 1.5 zilitolewa jimboni kwangu kwaajili ya kukarabati barabara kuna miradi mingi ya maji ambayo inatekelezwa jimboni kwa hiyo serikali inachapa kazi na wananchi waendelee kuiamini,” amesema
“Sasa hawa madiwani walipenda waje Dar es Salaam na mikoa mingine kuangalia utekelezaji kwa vitendo na kwa kweli wamefurahi na kumpongeza Rais Samia na CCM kwa kutekeleza Ilani ya chama kwa vitendo,”amesema Rweikiza
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa