May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabondia waoneshana ubabe Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MABONDIA zaidi ya 20 kutoka Mikoa ya Tabora, Morogoro, Kigoma, Mwanza na Shinyanga wameoneshana ubabe katika mashindano maalumu ya kusherehekea sikukuu ya krismas yaliyofanyika Mjini Tabora jana.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Chama Cha Ngumi Mkoa wa Tabora kwa lengo la kuinua vipaji yameleta hamasa kubwa kwa vijana na mashabiki wa mchezo huo Mkoani humo.

Akifungua mashindano hayo Afisa Utamaduni na Michezo wa Mkoa huo Hassan Katuli amepongeza ubunifu wa Viongozi wa chama hicho na kuahidi kuwatafutia vifaa vya michezo mabondia wa Mkoa huo ili kuinua vipaji vyao.

Amebainisha kuwa ushindani mkubwa uliooneshwa na vijana wa Mkoa huo katika mashindano hayo ni ishara tosha kwamba kama watawezeshwa vifaa watafika mbali zaidi na kuwa mabondia wakubwa.

‘Nawapongeza viongozi wa ngumi wa Mikoa yote iliyoshiriki mashindano haya, naamini kupitia mashindano hayo watapatikana wapinzani wa akina Dula Mbabe, Twaha Kiduku, Mwakinyo na wengine, nitawatafutia vifaa vya michezo’, amesema.

Katika mashindano hayo bondia Deusi Denis kutoka Kigoma amemchapa Sudi Moto wa Morogoro kwa KO raundi ya 3, bondia Hassan Boga wa Shinyanga akamtwanga bondia Ramadhan Twaha wa Tabora kwa KO pia.

Bondia Janga Denis wa Tabora amemtwanga Seleman Abdallah wa Morogoro kwa pointi na Shaban Abdallah wa Tabora akamtwanga Ngumi Kigazi wa Kgm kwa pointi huku Daud Mwita wa Mwanza na Awami Ramadhani wa Tbr wakitoka sare.

Katika mapambano mengine Jafar Juma wa Kgm amepata ushindi wa mezani baada ya Idd Msikozi wa Tbr kushindwa kutokea ulingoni kwa matatizo ya kifamilia na Salum Nzimile wa Kigoma akamtwanga kwa KO Maganga Francis wa Tbr.

Awali akikaribisha mabondia na viongozi walioambatana na wachezaji hao Mwenyekiti wa Chama Cha Ngumi Mkoani hapa Mwalimu Fred Msonga amesema mapambano hayo yamelenga kuinua vipaji na kuchochea jamii kupenda ngumi.

Ameongeza kuwa mapambano hayo yatakuwa yakifanyika mara kwa mara ili kuhamasisha vijana wengi kupenda masumbwi na kuahidi kuwa wataandaa tena mapambano ya namna hiyo siku ya pasaka.