May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kumekucha mbio za urafiki India, Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
 
MBIO za urafiki zitakazoshirikisha wanariadha kutoka nchini India na Tanzania zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho na keshokutwa jijini Dar es Salaam.
 
Mbio hizo zitahusisha kilometa tano na 10 na baadaye kufuatiwa na mbio za kilometa 120, kwenda Bagamoyo mkoani Pwani na kurudi Dar es Salaam, huku zikiongozwa na mkongwe wa riadha kutoka India, Milind Soman.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Balozi wa India hapa nchini, Binaya Srikanta Pradhan, amesema maandalizi ya bio hizo yamekamilika kwa kiasi kikubwa.
 
Amesema, anaishukuru serikali na Watanzania waliojiandikisha kushiriki mbio hizo ambazo lengo lake ni kuimarisha utamaduni kati ya Tanzania na India.
 
Hata hivyo amesema, mbio hizo zitahusisha wakimbiaji ambao ni raia wa Tanzania na India, usaili ulishafunguliwa huku kukiwa hakuna gharama za kujiunga.
 
Aidha, amesema wameandaa mbio hizo kuhakikisha wanadumisha umoja uliopo kati ya nchi hizo mbili ikiwemo wanariadha mbalimbali kubadilishana mawazo.
 
Pia, mwanariadha Soman ambaye kwa sasa ni mkufunzi wa mbio za riadha nchini India, atapata fursa ya kuzungumza na wanariadha mbalimbali kuhakikisha wanabadilishana uzoefu.
 
“Umoja wa India na Tanzania tumeandaa mbio za riadha ambazo zitafanyika kuanzia Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani na baadaye zitatoka Bagamoyo kurudi Dar es Salaam.

“Tutakimbia kilometa 120, pia tutakuwa na mkongwe Soman ambaye hivi sasa ni mkufunzi wa mchezo na msanii wa filamu nchini India,” amesema Balozi wa India nchini, Pradhan.
 
Naye mwanariadha Milind Soman, amesisitiza kuwa ameshafanya mbio kama hizo katika nchi mbalimbali na sasa ni zamu ya Tanzania na yupo tayari kukimbia.
 
“Ni fursa nzuri kwangu kutembelea Tanzania kuja kuiongoza timu itakayoshiriki mbio za riadha kwa pamoja, ambapo tutaungana na Watanzania mbalimbali lengo ikiwa ni kubadilishana uzoefu na kudumisha utamaduni uliopo kati ya nchi hizi mbili.
 
“Nimeshafanya safari kama hizi katika nchi mbalimbali Ulimwenguni, sasa ni zamu ya Tanzania, kuhakikisha tunafikia malengo.
 
“Tunafurahi na tunajivunia kuwakilisha Ubalozi wa India nchini Tanzania, kupitia mbio za riadha ninafikiri tutaacha alama kwa wenyeji,” amesema Soman.
 
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), William Kalaghe, amesema wamefarijika kuwa sehemu ya mbio hizo na waliunda kamati maalumu kuhakikisha wanafikia malengo.
 
Amesema, mbio hizo ni fursa ya kuutangaza mchezo wa riadha zaidi na zinatarajiwa kuwa endelevu kwani zitafungua milango kwa wadau wengi wa mchezo huo.
 
“Tunashukuru kwa kujumuishwa kuwa sehemu ya maandalizi ya mbio hizi ambazo zinafanyika Tanzania kwa mara ya kwanza, hivyo tunatarajia zitakuwa endelevu na wanariadha mbalimbali watanufaika nazo,” amesema Kalaghe.