May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lucas: Fichueni taarifa za ukatili wa kijinsia

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

AFISA Ustawi  wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake  na Makundi Maalum, Baraka Lucas amesema kutokana na kuwepo kwa mifumo  mingi ya utoaji wa taarifa za ukatili wa kijinsi imesaidia kwa kiasi kikubwa watu kufichua vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia na kuchukuliwa hatua.

Miongoni mwa mifumo ya utoaji wa taarifa inayotumika ni pamoja na mabaraza ya wazee,Kamati za Ulinzi na Usalama kwa mwanamke na Mtoto,Mabaraza ya watoto  katika Shule pamoja na watoa huduma kwa ngazi ya Jamii.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam katika maonesho ya 46 ya Sabasaba,Lucas amesema miaka ya nyuma watu walikuwa hawatoi taarifa  za vitendo vya ukatili wa kijinsia kutokana na mifumo hiyo kutokuwa rafiki lakini sasa watu waendelee kutoa taarifa hizi ili ziweze kuwabaini waarifu.

Amesema  watu wameweza kubaini mifumo hiyo na kuweza kuitumia ipasavyo kwa kutoa taarifa dhidi ya vitendo hivyo na kujua wapi wanaweza kusaidia jamii.

“Vitendo hivi vinavyopelekea kushamiri ni matokeo  ya watu kupata athari mbalimbali ikiwempo mtu labda aliwahi kutendewa na sasa kuamua kulipiza,na wengine ni kutokana na hali ya maisha ,”amesema na kuongeza

“Ukatili unaofanyika unaweza kuwa wa kisaikolojia,kimwili au uchumi  na asilimia kubwa ya watu wanaokutana navyo vitendo hivi ni wanawake na watoto kwa sababu kundi hili limekuwa na nafasi ndogo ya kujitetea,”amesema

Kwa Upande wake Mratibu wa Kitengo cha Elimu,Ushauri na Msaada wa Kisheria kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii,Rufina Khumbe amesema taasisi yao imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inatoa elimu juu ya masuala ya vitendo vya ukatili wa kijinsia,Huduma za Afya pamoja na kutoa ushauri kwa wanafunzi na watu mbalimbali wanaofika katika kituo chao.

Amesema wamekuwa wakitembelea shule na vyuo mbalimbali pamoja na makanisa katika kutoa elimu hizo mbalimbali kwa kufanya hivyo wamekuwa wakiwafikia watu wengi zaidi.

“Huduma yetu tunayotoa katika vituo vyetu kikiwemo cha Kijitonyama ni bure kabisa na kipo kwaajili ya watu wote sio kwa wanafunzi pekee yao,tumeweza kufika katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha tunawajengea uwezo watu kwa kutoa elimu ya afya ya uzazi wa mpango ,magonjwa ya Ukimwi pamoja na Magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yanaathiri watu wengi kutokana na mpangilio wa chakula,”amesema 

Amesema wameshiriki maonesho ya 46 ya Biashara Sabasaba na kutoa fursa za ushauri na nasaha ambapo zaidi ya watu 130 wameweza kufika katika banda lao na kujifunza mambo mbalimbali pamoja na kupokea ushauri na nasaha.

“Watu ni wengi wanafika katika banda letu na wanajifunza vitu mbalimbali na kupokea ushauri na nasaha miongoni mwa vivilivyoonekana kutolewa kwa watu hao ni pamoja na ushauri na nasaha juu ya migogoro ya familia, masuala ya ukatili pamoja naushauri wa hali za msongo wa mawazo.