September 26, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LHRC yaanda marathon ya siku ya haki za binadamu

Na Mwandishi wetu,timesmajira online Dar

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu( LHRC) kimeandaa mbio maalum zitakazojulikana kama haki marathon ambapo zaidi ya watu 1000 wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo kupitia njia  ya mtandao.

Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Octoba 17 hadi Desemba 10  kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya Kimatafa ya haki za binadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es salaam, Mkurungezi Mtendaji (LHRC ),Anna Henga amesema lengo la mbio hizo  ni kujenga uelewa na kuwawezesha watanzania kutambua wajibu wao wa kulinda haki za binadamu nchini.

Amesema kutokana na kuwepo kwa janga la UVIKO 19,LHRC imelazimika kuratibu marathoni kwa njia tofauti kwa kuzingatia miongozo ya kiafya inayohimiza kuepuka misongamano mikubwa .

“Mbio hizi zitatoa fursa kwa mtu yoyote kushiriki ili mradi awe amejisajili na kulipia pia mbio hizi zinatarajiwa kudumu kwa muda wa wiki saba ambapo watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi nje na ndani wataweza kushiriki kwa kasi watakayochagua na wakati watakayochagua wenyewe”amesema

Henga ameeleza kuwa mbio zitakuwa katika makundi matatu ambayo ni kilometa 21, Kilometa 10 na Kilomenta 5 ambapo baada ya kumaliza washiriki kutegemea eneo lake ataelekezwa wapi na wakati gani wa kwenda kuchukua medali zao.

Aidha amesema mbio za haki marathon zitatafakarisha umma wa watanzania juu ya jukumu la kila mmoja kulinda na kuheshimu haki za binadamu.

Kwa upande wake Mratibu wa Haki Marathon Deus Ntukamazima amesema mkimbiaji katika mbio hizo atatakiwa kujisajili moja kwa moja katika tovuti ya Haki marathon .

Amesema mkimbiaji atapaswa kuwa na simu janja ambayo kwani baada ya kumaliza kukimbia tovuti ya Haki marathon itaweza kuoenesha ni kwa kiasi gani amekimbia.