April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kupitia TCCP waandishi wanolewa, juu ya ugonjwa wa saratani


Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

IMEELEZWA kuwa wagonjwa wengi wa saratani wanafika katika vituo vya kutolea huduma wakiwa katika hatua mbaya,kutokana na kukosekana kwa taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo kwa jamii.

Hivyo kupitia mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) ambao unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na Aga Khan Foundation (AKF) , waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna ya  kuripoti habari zinazohusiana na ugonjwa wa saratani kwa usahihi.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza juu ya namna ya kuandika habari sahihi za afya hususani za ugonjwa wa saratani,Meneja Ubia,Uwezeshaji na Mawasiliano wa mradi wa TCCP Dkt.Sarah Maongezi amesema, miongoni mwa changamoto katika huduma za saratani nchini hapa ni pamoja na wagonjwa wengi kufika katika hospitali wakiwa katika hatua za mwisho.

Ambapo kubwa zaidi ni  uelewa na elimu ndogo katika jamii  juu ya saratani huku  mradi huo unatarajia kuwanufaisha watu milioni 1.7, ikiwemo waandishi wa habari ambao wamewapatia elimu sahihi juu ya saratani hivyo  wataweza kufikisha taarifa sahihi kwa jamii  kwani inawaamini pia wanauwezo wa kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja.

“Wagonjwa wengi  wa saratani wanafika katika hospitali zetu wakiwa katika hatua ya tatu na ya nne,lakini uelewa mdogo katika jamii nina hakika ninyi waandishi wa habari mnajua,pia uhaba wa mashine za tiba ya saratani kuuzwa bei ghali,kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mashine 1 inapaswa kuhudumia watu milioni Moja na hapa nchini tupo milioni 60 tuna mashine 7 tu,” amesema Dkt.Maongezi.

Daktari Bingwa wa upasuaji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, Dkt.Athanas Ngambakubi,akitoa elimu juu ya saratani kwa waandishi wa habari hao, amesema kwa mwaka 2020 inakadiriwa watu milioni 1.1 walipata saratani.

Huku watu 711,429 waliofariki kwa saratani Afrika wakati huo Tanzania watu 40,464 walipata saratani  kati yao 26,945 walifariki kutokana na saratani.

“Hivyo amesema nchini hapa saratani inayoongeza ni ya mlango wa kizazi,matiti na tezi dume,hivyo katika kupambana na ugonjwa huo,wenzetu Aga Khan,wameamua kuja na mradi huo,”

Awali akifungua mafunzo hayo  Daktari  Bingwa wa magonjwa ya saratani hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt. Beda Likonda,amesema ipo mihimili minne ambayo ikitendewa haki  jamii itafikiwa na kuleta matokeo chanya ikiwemo takwimu,elimu,tiba na tiba shufaa

Dkt .Likonda amesema wanatakiwa kutoa elimu kwa jamii,wafanyakazi na wadau wa sekta ya afya,ili wajue saratani ni nini, inatokana na nini,jinsi gani ya kujizuia na je,wafanye nini  na wakipata wagonjwa waweze kuwatibu.

Pia amesema,serikali ihakikishe  tiba zinapatikana kuanzia katika hatua mbalimbali za vituo vya tiba kama vile vituo vya afya, zahanati,hospitali za mikoa na wilaya ili huduma ziwafikie wananchi.

Aidha amesema,mhimili wa nne ni tiba shufaa ambayo mgonjwa anarudi nyumbani hana uwezo wa kumtibu,hata kama atafariki asiwe kwenye matatizo mengi.

“Katika mihimi hiyo ya kupambana na adui yetu saratani,kuna mapungufu mengi,nimefurahi wenzetu wa Aga Khan na Wafaransa wameungana kuona tunaifikia vipi hii mihimili minne,wameanza na mihimili miwili watatusaidia katika kujenga na kuhakikisha mihili yote mine inakamilika ili tuweze kupigana vizuri na saratani (adui yetu),”amesema.