Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Korogwe
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Wazo Mwang’onda amepongeza ujenzi wa Mradi wa Maji Gombero- Mapangoni kwa kusema utawaondolea wananchi adha na kuwawezesha kupata maji safi na salama.
Amesema hayo Juni 27, 2026 alipofika kuweka Jiwe la Msingi la mradi huo uliopo Kijiji cha Mapangoni, Kata ya Kerenge, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
“Mradi wetu ujenzi wake unaendelea vizuri, tenki limejengwa vizuri na linapokea maji kwa wingi sana, na wananchi wamefungiwa zaidi ya DP (Vilula) 20 ambazo zinapeleka maji kwa wananchi wa Kijiji cha Mapangoni na Kijiji cha Gombero.

“Namshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta fedha nyingi kuja kujenga mradi mkubwa huu wa maji. Wakati anaingia madarakani, aliahidi kwenda kumtua ndoo kichwani mwanamke, na wote tumeshuhudia kwa macho sisi wenyewe na akileta mapinduzi makubwa kwa kupeleka maji karibu na makazi ya watu” amesema Mwang’onda.
Mwang’onda amesema anachokiomba Rais kutoka kwa wananchi ni kuilinda amani, kwani ili aweze kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi ni lazima nchi iendelee kuwa na amani, utulivu, umoja na mshikamano.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Korogwe Mhandisi Muharami Mohamed amesema Mradi wa maji Gombero Mapangoni ulianza kutekelezwa Agosti 24, 2022 na unatarajiwa kukamilika Agosti 10, 2026 kwa kutumia Mkandarasi M/s BEZALEL CONSTRUCTION CO.LTD wa Dar es Salaam. Lengo la mradi huo ni kutekeleza adhma ya Serikali ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi wapatao 3,663 wa vijiji vya Gombero na Mapangoni, ambapo mradi huo upo asilimia 90 na umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
“Gharama ya mradi huu ni sh. 914,630,518 kupitia fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF) na fedha za Lipa kwa Matokeo (PforR). Hadi sasa jumla ya sh. 609,675,390 zietumika. Kazi zilizopangwa na kutekelezwa kwa mujibu wa mkataba ni ujenzi wa chanzo cha maji kwa asilimia 90, ujenzi wa tangi la maji lenye ujazo wa lita 100,000 linalohudumia Kijiji cha Mapangoni kwa asilimia 95.

“Ujenzi wa tangi lenye ujazo wa lita 75,000 linalohudumia Kijiji cha Gombero kwa asilimia 95, ujenzi wa BPT moja kwa asilimia 95, uchimbaji wa mtaro na kufukia bomba mita 25,694 kwa asilimia 98, ujenzi wa vilula (DPs) 20 kwa asilimia 98, kuweka alama za bomba 217 kwa asilimia 80, na ujenzi wa valve chamber 20 kwa asilimia 50” amesema Mhandisi Mohamed.
Mhandisi Mohamed amesema kwa niaba ya wananchi, wanamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuondoa kero ya maji kwa wananchi wa vijiji vya Gombero na Mapangoni, pia kwa kuwezesha wananchi zaidi ya 90 kupata ajira ya muda katika kipindi chote cha utejelezaji wa mradi.

“Ili mradi huu uwe endelevu wananchi wameshirikishwa katika hatua zote za utekelezaji na kwa sasa kipo Chombo cha Kijamii cha Watumia Maji (CBWSO) kama ilivyoainishwa kwenye Sheria Na 5 ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019. Chombo hiki cha kijamii kitatekeleza shughuli zote za uendeshaji na matengenezo ya mradi huu” amesema Mhandisi Mohamed.




More Stories
Exim yatoa madawati 80 shule ya msingi
Jubilei ya Dhahabu ya Sabasaba yazinduliwa kwa kishindo
Twange afichua kilichosababisha hitilafu ya umeme