May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kinana: Rais Dkt.Samia amedhamiria kwa dhati uchaguzi huru na wa haki

Na Penina Malundo, PemimamalundoOnline,Dar

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi Mkuu wa 2025, unakuwa huru na haki.

Ameenda mbali zaidi na kusisitiza kwamba hakuna sababu ya Watanzania hasa asasi za kiraia, viongozi wa dini pamoja na vyama vya siasa kuwa na hofu na chaguzi hizo.

Kinana aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia, kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha ACT -Wazalendo.

Kinana alisema kuna sheria na dhamira, hivyo unaweza kuwa na sheria nzuri, lakini kama huna dhamira nzuri, unaweza kukanyaga ile dhamira na ukafanya unavyotaka.

“Unaweza kuwa na dhamira nzuri na sheria mbaya, dhamira ikitawala mambo yanakuwa mazuri,” alisema Kinana na kuongeza;

“Rais Samia ameamua uchaguzi wa mwaka huu na mwaka ujao kwamba utakuwa huru na wa haki, wakati ninazungumza hivi nina uhakika wapo watu wana mashaka na kauli hii na hao wenye mashaka wanazo sababu na sababu zao zinatokana na mwaka 2019/2020, huo ndio ukweli.”

“Sheria tuliyokuwa nayo katika uchaguzi wa 2025 iliwezesha wanachama kutoka upinzani 117 kuingia Bungeni, sheria hiyo hiyo iliwawezesha madiwani asilimia 40 kuingia katika nafasi za halmashauri ,tulipokuja 2020 msema kweli mpenzi wa Mungu, lazima tuseme kweli,” alisema.

Alisema hofu ya Watanzania na hofu ya vyama vya siasa, asasi za kiraia na baadhi ya viongozi wa dini msingi wa hofu yao ni yale yaliyotokea 2020.

Kinana alisema Rais Samia, ameamua uchaguzi huu utaachiwa wapiga kura ambao ndio uchaguzi wao na utoe taswira, kwani hata wabunge kukubali kufanya marekebisha ya Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi maana yake tunakwenda katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadaye mwakani uchaguzi mkuu.

Kuna maoni yametolewa na wadau mbalimbali katika Kamati za Bunge, bungeni…ukiangalia sheria ile baada ya maoni na ushauri kuna mabadiliko makubwa sana,” alisema Kinana na kuongeza;

“Nataka niwahakikishie kwamba Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dkt.Samia, ina dhamira ya dhati kwa mwaka huu wa uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka ujao ili kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki,” alisema Kinana.

Alisema mbali na kupitisha sheria nzuri za kuhakikisha kunakuwapo uchaguzi huru na wa haki, pia dhamira ya Rais Dkt.Samia kufanikisha hilo inajipambanua katika utekelezaji wake.

Rais Samia Suluhu Hassan

Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar,alisema imetokana na mazungumzo ya viongozi wa CCM na Serikali yake na viongozi wa Chama cha Act wazalendo, chini ya uongozi madhubuti na imara wa Maalim Seif Sharif Hamad.

Alisema baada ya mazungumzo hayo yalifatiwa na kura ya maoni ya wananchi na sio maoni ya vyama vilipendekeza kuwa na serikali hiyo, bali ilikuwa ni maamuzi ya wananchi ambao waliunga mkono kwa asilimia zaidi ya 60.

“Baada ya kura ya maoni ya wananchi, serikali iliweka mfumo huo katika katiba, hakuna wa kuiondoa Serikali hii bila kura nyingine ya wananchi, haitakuwa uamuzi wa CCM wala ACT Wazalendo, bali utakuwa ni uamuzi wa wananchi,”‘alisema Kinana na kuongeza;

”Niwahakikishie CCM inathamini ushirika wenu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ,tunatambua katika serikali ya umoja wa kitaifa wakati mwingine mambo hayawezi kwenda kwa urahisi, lakini tupo tayari kukaa nanyi, kusikilizana nanyi kwa maslahi mapana ya kutafuta haki, uhuru na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar,”alisisitiza.

Katika hatua nyingine Katibu wa Itikadi na Uenezi na Mafunzo CCM, Paul Makonda, amesema Rais Samia, ameridhia kutenga siku moja kila mwezi wa ajili ya kusikiliza kero za wananchi mmoja mmoja.

Makonda aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara alizozifanya hivi karibuni kwenye mikoa 23.

Alisema hatua ya Rais Samia, kuamua kusikiliza kero za wananchi inatokana na msingi wa katiba ya CCM na ilani na matakwa ya hali ya sasa.

“Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kulipatanisha Taifa na kuleta faraja, matumani pamoja na kumsikiliza mtu na kumpa nafasi ya kushiriki katika kujenga Tanzania yake bila kujali kipato,elimu na nafasi yake,”alisema

Makonda alisema kupitia ziara yake aliyoifanya hivi karibuni, imeibua mambo mengi na kuonesha kiu ya wananchi kuongea na viongozi wao na kupata faraja wanapokutana na viongozi wao na kupata majibu.

Makonda alisema Rais Dkt Samia ni muumini wa masikilizo, ameamua kutenga siku moja ya kila mwezi kuwasikiliza wananchi.

Alisema lengo la kuwasikiliza wananchi ni kudumisha na kuzidhihirisha kwa vitendo kwamba anataka viongozi aliowateua wasikilize kero za wananchi na kuzitatua.

“Mwananchi atakayepata nafasi ya kumuoma Samia katika ofisi zetu za Chama za Dodoma , Dar es Salaam au Zanzibar ataulizwa kama amewasilisha kero zake kwa watendaji,”alisema

Aidha, alisema ameamua kufanya hivyo kama kumuenzi hayati Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, kwa vitendo kwa mema aliyoyafanya kwa uhai wake