Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar
ZIARA ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha imeacha ujumbe mmoja mkubwa uliovuka mipaka ya siasa za vyama; umuhimu wa kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Katika siku zote za ziara hiyo, Kihongosi hakujikita tu katika kukagua miradi ya maendeleo, kuangalia uhai wa chama na kusikiliza kero za wananchi, bali ametumia majukwaa mbalimbali kuwakumbusha watanzania kuwa maendeleo yoyote yanayopatikana nchini yanategemea uwepo wa amani.
Akiwa katika wilaya mbalimbali za Siha, Moshi, Hai, Hanang, Babati, Simanjiro na Karatu, amesisitiza mara kwa mara kuwa Watanzania wanapaswa kuwa makini na kauli za baadhi ya wanasiasa wanaojaribu kuwashawishi wananchi kuichukia nchi yao, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na kuhamasisha vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa Taifa.

Kwa mujibu wa Kihongosi, historia inaonesha kuwa mataifa mengi yaliyokuwa na uchumi imara na rasilimali nyingi yamejikuta yakipoteza mwelekeo baada ya kuruhusu migogoro, vurugu na machafuko kutawala. Ndiyo maana ameeleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani Afrika kutokana na maamuzi ya viongozi wake pamoja na utayari wa wananchi kulinda umoja wao.
Ujumbe huo umeenda sambamba na kazi alizokuwa akizifanya katika maeneo mbalimbali aliyotembelea. Katika Mkoa wa Kilimanjaro amekagua miradi katika Sekta ya Elimu na Afya ikiwemo Shule ya Wasichana ya Kilimanjaro, Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza ya Kibong’oto, Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi pamoja na mradi mkubwa wa stendi ya mabasi ya Ngangamfumuni. Lakini pia amekagua miundombinu ya barabara nk.
Katika kila mradi aliokagua, amesisitiza kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali una maana pale tu amani inapodumu. Ameeleza kuwa shule, hospitali, barabara, stendi na miradi mingine ya maendeleo haiwezi kuwa na manufaa ikiwa nchi itakumbwa na migogoro au vurugu.
Ujumbe huo uliendelea kujitokeza akiwa Mkoa wa Manyara ambapo pamoja na kukagua miradi ya maji, afya, elimu na majengo ya utawala, aliwataka wananchi kutokubali kushawishiwa na watu wanaotaka kutumia siasa za uchochezi kwa maslahi yao binafsi.

Akiwa Hanang, Babati na Simanjiro, Kihongosi amesisitiza kuwa maandamano, vurugu na migogoro havijawahi kuwa suluhisho la maendeleo ya wananchi. Badala yake amewahimiza wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali, kuilinda miundombinu ya umma na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Moja ya hoja zilizojitokeza kwa nguvu katika ziara hiyo ni kwamba, wananchi ndio waathirika wakubwa katika uvunjifu wa amani. Ameeleza kuwa mara nyingi wanaohamasisha vurugu huendelea kuwa salama, lakini madhara yake hubebwa na wananchi wa kawaida ambao familia zao, biashara zao na maisha yao yote yapo hapa nchini.
Wakati huo huo, ziara hiyo imeonesha sura nyingine ya uongozi inayozingatia usikivu wa wananchi. Katika maeneo mbalimbali, Kihongosi amepokea kero za wananchi, ametoa maelekezo ya kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali na nyingine kuzifikisha kwa mamlaka husika. Ametoa maelekezo kuhusu mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, pia amefuatilia changamoto za usafiri Hanang, pamoja na kuhimiza upatikanaji bora wa huduma za afya na elimu.
Aidha, Kihongosi ameonesha kuwa siasa zinaweza kutumika kujenga matumaini kwa wananchi, pale aliposhiriki kutatua changamoto za watu wenye mahitaji maalumu na kuhamasisha viongozi kusikiliza wananchi wakati wote badala ya kusubiri kipindi cha uchaguzi.

Kwa ujumla, ziara ya Kihongosi katika mikoa ya Kaskazini haikuishia kwenye masuala ya chama pekee, bali ilibeba ujumbe mpana wa kitaifa kwamba maendeleo yanahitaji amani, umoja na mshikamano. Ujumbe wake ulikuwa wazi kuwa Watanzania wanapaswa kuendelea kulinda tunu hiyo adimu kwa kukataa kauli za uchochezi, kuheshimu vyombo vya ulinzi na usalama, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuendelea kuijenga Tanzania yenye utulivu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Katika nyakati ambazo dunia inashuhudia migogoro katika maeneo mbalimbali, Tanzania ina kila sababu ya kuendelea kuilinda amani yake. Huo ndio ulikuwa moyo wa ziara ya Kenani Kihongosi Kaskazini mwa Tanzania, kwamba amani si jambo la kawaida, bali ni msingi mkuu unaobeba maendeleo yote ya Taifa.
MAPENZI YA WANANCHI KWA CCM
Katika Mikoa yote aliyopita Kihongosi katika ziafa yake, imeonesha wazi wazi kuwa wananchi kuwa na imani na Chama hicho tofauti na vyama vingine vya upinzani.
Wananchi wamejitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara iliyofanywa na mwenezi huyo wa CCM katika Wilaya mbalimbali za mikoa hiyo ya Kaskazini, wengi wakiwa na lengo la kusikiliza sera pamoja na kuwasilisha kero zao kwa chama hicho, wakiamini kuwa ndicho kinachoweza kuwatatulia.

Aidha baadhi ya wananchi waliofika katika mikutano hiyo, wameeleza kuvutiwa nayo wakieleza kuwa, CCM imekuwa ikifanya siasa zinazoleta matokeo kwa wananchi kwa kunadi chama pamoja na utekelezaji wa ilani yake, jambo ambalo wananchi wanapendezwa nalo na si kufanya siasa za malalamiko zisizokuwa na ufumbuzi wa matatizo ya watanzania.
KAZI NA UTU WA CCM
Kauli mbiu ya CCM ya ‘Kazi na Utu’ imeendelea kuoneshwa na chama hicho kupitia Kihongosi, ambaye amekuwa si tu akikagua miradi ya maendeleo bali akiwatatulia watu changamoto zao ikiwemo binafsi na za maendeleo ya kijamii.
Kihongosi ametoa misaada mbalimbali baada ya wahitaji kuomba kupitia mikutano yake ikiwemo ada za shule, kutoa msaada wa makazi, pesa taslimu pamija na kutatua migogoro ya ndoa. Pia kutatua changamoto zinazohusisha sekta mbalimbali Serikalini.
SIASA NA USANII
Kati ya vitu vinavyowavutia watu wengi ni pamoja na siasa zinazofanywa na Kihongosi akizipamba na burudani ya muziki, jambo ambalo limefanya mikutano yake kuhudhuriwa na watu wa rika zote ikiwemo wazee na vijana.
Kihongosi amekuwa akitoa burudani ya ‘kuchana mistari’ jukwaani baada ya kumaliza kuhutubia wananchi, kitu ambacho wengi wao wameeleza kuwa na mvuto wa aina yake tofauti na walichokiita ‘siasa serious’ kusema kuwa zinachosha na kusema kuwa zimepitwa na wakati.


More Stories
Jinsi umaskini,ukosefu wa mabweni unavyowanyima watoto wenye mahitaji maalumu haki ya elimu
CAMFED Ilivyobadili maisha ya wasichana Tanzania
Maisha ya machozi yageuka matumaini