Na Judith Ferdinand
SAA 12 alfajiri, kabla hata mwanga wa jua haujafunika anga la Nyasasa B, Kata ya Kawekamo wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Debora Manyama maarufu kama Bibi Ayubu huanza safari nyingine ya kila siku.
Mkono mmoja amemshika mjukuu wake, Ayubu Jackson (14) mwanafunzi wa darasa la nne, huku mkono mwingine akiwa amebeba mahitaji madogo ya shule. Mbele yao kuna safari ya saa moja kwa miguu kuelekea Kituo cha Elimu Maalumu Huruma, kilichopo Kata ya Kawekamo.

Kwa watu wengi, kutembea kwa saa mbili huweza kuonekana jambo la kawaida. Lakini kwa Bibi Ayubu mwenye umri wa miaka 60, anayemlea mjukuu mwenye changamoto ya ulemavu tofauti, safari hiyo ni mzigo mzito unaobeba matumaini ya maisha ya mtoto huyo.
“Natumia karibu saa moja kumpeleka shule na saa moja kumrudisha. Wakati mwingine anakuwa msumbufu njiani, hivyo lazima niwe naye muda wote,” anasema Bibi Ayubu.
Simulizi ya Ayubu na bibi yake si ya familia moja pekee,ni kioo cha changamoto zinazowakabili mamia ya watoto wenye mahitaji maalumu nchini Tanzania.Licha ya jitihada za Serikali kuimarisha elimu jumuishi,lakini umaskini,ukosefu wa mabweni, usafiri na miundombinu rafiki bado unaendelea kuwa kikwazo kikubwa cha upatikanaji wa elimu kwa usawa.
SAFARI YA AYUBU
Safari ya Ayubu haikuwa rahisi tangu utotoni,akiwa na umri wa miaka mitano, alikataliwa na ndugu wa upande wa baba baada ya kuanza kuanguka kifafa mara kwa mara huku hali yake ikiwa mbaya.
“Alikuwa amechubuka mwili mzima. Tulipofika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, madaktari walikuwa wanahoji chanzo cha tatizo.Mama yake baada ya kuona maswali yamezidi aliondoka kabisa na kumuacha,” anasimulia Bibi Ayubu.
Anasema alikaa hospitalini hapo na Ayubu kwa miezi mitatu,lakini baadae madaktari walibaini kuwa mbali na kifafa na kuchubuka mwili aligundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu (TB),ambao alitibiwa kwa muda wa miezi sita.
Baada ya matibabu hayo, Ayubu alipona na kuanza safari mpya ya maisha kupitia elimu baada ya madaktari kumuunganisha na shirika moja ambalo lilimtafutia shule ambayo ni Kituo cha Elimu Maalumu Huruma, ambacho kimejikita kutoa huduma ya elimu,mazoezi ya viungo na stadi za maisha kwa watoto wenye ulemavu mbalimbali.
Lakini changamoto hazikuishia hapo. Mama yake aliondoka na kumuacha mikononi mwa bibi yake, ambaye tayari alikuwa na majukumu mengine ya kifamilia.Leo hii, Bibi Ayubu ndiye mlezi mkuu wa Ayubu pamoja na wadogo zake wawili.

ELIMU INAYOLIPIWA KWA JASHO LA BIBI
Kila siku ya masomo huanza na maandalizi mazito.Bibi Ayubu humuandaa Ayubu, na wakati huohuo huwahudumia wadogo zake wawili wanaosoma chekechea.
Nyumbani kwake pia kuna wagonjwa wengine wawili ambao ni mume wake anayesumbuliwa na pumu na mdogo wake aliyepooza kwa kupata kiharusi.Huku akitafuta riziki kwa ajili ya kulisha familia na kununua dawa
Bibi Ayubu, anasema kipato chake kinatokana na biashara ndogo ya mayai na mbogamboga,lakini karibu kila siku hupoteza takribani saa mbili kwa ajili ya kutumia kumpeleka shule na kumrudisha nyumbani Ayubu, hali inayodhoofisha biashara yake.
“Faida ya siku inaweza kuwa shilingi 1,000, 2,000 au 3,000. Ukipata huwezi kununua mkaa 1,000,hivyo maisha yangu natumia kuni sijui mkaa wa gesi.Nikipata 2,000 nanunua unga na dagaa tunakula mlo mmoja tu kwa siku badala ya mitatu,”anasema Bibi Ayubu.
MAZINGIRA HATARISHI NYUMBANI NA NJIANI
Lakini ugumu wa maisha ya Bibi Ayubu hauishii kwenye kipato kidogo. Mazingira anayoishi nayo pia yanaongeza hatari kubwa kwa maisha ya mjukuu wake.
Nyumba wanayoishi katika mtaa wa Nyasasa B imebomoka upande mmoja, na kuacha matofali yaliyodondoka yakitapakaa nje ya nyumba.Kwa mtoto mwenye kifafa, mazingira haya ni tishio la moja kwa moja.
Hakuna eneo la kutosha la kuchezea au kutembea kwa uhuru. Miti mingi imeizunguka nyumba, huku njia zikiwa nyembamba na zisizo salama.
“Ayubu anachangamoto fulani,aliwai kudondoka akaangukia jiwe ambalo lipo hapo nje akapasuka juu kidogo ya jicho,hivyo nilimpeleka kituo cha Afya Buzuruga,wakampatia matibabu kwa kumshona na maisha yakaendelea,” anasema Bibi Ayubu.
Njia ya kuelekea barabarani imejaa majani na haina miundombinu rafiki. Ngazi katika nyumba hiyo hazijajengwa kwa kuzingatia mahitaji ya Ayubu, hivyo humlazimu kutegemea msaada wa bibi yake au mtu mwingine.
Barabara ya kuelekea shuleni pia si salama, ikiwa na vumbi na magari pamoja na pikipiki zinazopita kwa kasi.Kutokana na hali yake Ayubu ana nguvu kuliko bibi yake ambaye ni mzee kwa sasa,humpa shida pindi anapost mlazimisha kumtembeza barabarani kwani kuna muda anagoma hali inayoongeza hatari ya ajali na usalama.

SAFARI INAYONYIMA FURSA
Kwa Ayubu, changamoto ya elimu haianzi darasani,inaanza njiani.Kutokuwa na usafiri wa uhakika kunamaanisha muda mwingi anaotakiwa kwa kujifunza hutumika kutembea.
“Ningeweza kufanya biashara yangu kwa uhuru huku Ayubu akipata elimu bila usumbufu.Changamoto ninapokuwa kwenye biashara mara napigiwa simu nikamfuate shuleni,pia wadogo zake ambao wapo chekechea inakuwa kazi ngumu kwangu kuwapeleka na kuwarudisha na hapo nakuwa sijawapikia chakula ukizingatia nina wagonjwa wengine,”anasema Bibi Ayubu.
UKOSEFU WA MABWENI UNAVYOZIDISHA TATIZO
Changamoto ya usafiri inafungamana moja kwa moja na ukosefu wa mabweni katika shule nyingi za watoto wenye mahitaji maalumu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA),Walter Miya, anasema
taasisi hiyo imeingia makubaliano na Kituo cha Elimu Maalumu Huruma,kwa ajili ya kuangalia watoto wenye mahitaji maalumu waliopo shuleni hapo,ambapo
wameweza kuzibainisha familia 10 ikiwemo familia hiyo ya kina Ayubu Jackson,ambaye anatumia muda mrefu kuifua elimu kituoni hapo.
Hivyo ni muhimu kwa shule na vituo kama Huruma kuwezeshwa mabweni ,ili watoto kama Ayubu waweze kupata haki ya elimu kwa ukaribu.
“Tunaendelea kuomba Serikali kuangalia suala la bweni kwa watoto wenye mahitaji maalumu kwa jicho la tatu,kwani yangesaidia watoto hao kupata muda wa ziada wa kujifunza na kupunguza changamoto za safari,” anasema Miya.

WATOTO WANAORUDI NYUMBANI NA KUANZA UPYA
Katika Kituo cha Elimu Maalumu Huruma, changamoto ya mabweni inaonekana kwa macho.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Boniventure Toto, anasema watoto wengi hupoteza maendeleo yao wanaporudi nyumbani.
“Wapo wazazi wanaoamini watoto hawawezi kujifunza. Wengine wanawafungia ndani wanaporudi nyumbani.Bila mabweni, mtoto anaporudi nyumbani anaweza kusahau alichojifunza na anaporudi shule huanza upya,”anasema Toto.
ELIMU INAYOBADILISHA MAISHA
Licha ya changamoto, elimu maalumu inaleta mabadiliko makubwa.Katika Kituo cha Elimu Maalumu Huruma, watoto wengi wameonesha maendeleo makubwa.
Toto anasema mazoezi ya viungo, stadi za maisha na uangalizi wa walimu yamekuwa msingi wa mabadiliko hayo.
“Wapo watoto waliokuwa hawawezi kushika kikombe cha uji, leo wanakunywa wenyewe. Wengine waliokuwa hawawezi kutembea, sasa wanaweza kusimama na kutembea hatua chache,”anasema Toto na kuongeza:
“Wamejifunza kufua, kuosha vyombo, kumwagilia bustani na kujihudumia. Wengi ambao wamepita katika kituo hiki sasa wako sekondari na vyuo vikuu.Mwaka jana kuna watoto wetu wamechaguliwa kwenda VETA Tabora,kwa ajili ya kuendeleza ujuzi tuliowapa hapa,”.
Na hii inaonesha kuwa elimu sahihi inaweza kubadilisha maisha kabisa.
SERIKALI YASEMA ELIMU NI HAKI YA KILA MTOTO
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Baraka Makona, anasema elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto na Serikali inaendelea kuwatambua watoto wenye ulemavu ili kuwapatia huduma za elimu na afya.
“Mtoto yoyote haijalishi hana au ana ulemavu wowote lazima apewe haki yake ya msingi ya kupata elimu pamoja na haki nyingine zote.Hii imeelezwa kwenye Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto,Sheria ya Mtoto sura namba 13 kuhusiana na elimu jumuishi,Sheria ya Elimu pamoja na kwenye Uratibu wa Muongozo wa Watoto wenye Ulemavu,”anasema Makona.
Anasema pia wazazi wanapaswa kuwapeleka watoto shule badala ya kuwaficha nyumbani.

TAKWIMU ZILIZOIBUA MASWALI
Ofisa Elimu Maalumu Mkoa wa Mwanza, Meshack Masanja, anasema kuna shule 441 zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu 5,492.Wasichana 2693 na wavulana 2,799,huku katika shule hizo ni shule 12 pekee zenye mabweni 12 kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu.
Anakiri pia kuwepo kwa uhaba wa walimu wa elimu maalumu,ambapo anasema kwa shule hizo zilizopo mkoani Mwanza kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu zina walimu wanaofundisha lugha ya alama 83 tu,kati yao wanaume 50 na wanawake 33.
“Changamoto kubwa inayokwamisha utekekalezaji wa elimu jumuishi ni uhaba wa walimu hususani katika aina kuu tatu za wenye ulemavu ikiwemo watoto wenye changamoto ya afya ya akili. Serikali kwa kushirikiana na taasisi zake pamojaj na Idara ya Elimu Mkoa wa Mwanza tunaendelea kupambania hupatikanaji wa walimu hao,”. anasema Masanja.
Kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF ya Novemba 2021 inaonesha kuwa kuna watoto milioni 240 wenye ulemavu duniani huku asilimia 49 hawajawahi kuingia shule.Hii inaonesha ukubwa wa changamoto ya elimu jumuishi duniani.
Masanja anasema,Serikali na Mkoa inafanya kazi mchana na usiku kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma,kama malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 yanavyoelekeza.
Huku akionya walimu wanaovunja Sheria ya Elimu na Sheria ya watu wenye ulemavu namba 9 ya mwaka 2010, kwa kuwakataa watoto wenye mahitaji maalumu kuanza masomo katika shule husika.
Hata hivyo wakati Tanzania ikiendelea kusisitiza elimu jumuishi, simulizi ya Ayubu inaonesha pengo kati ya sera na uhalisia.Ukosefu wa mabweni, usafiri na miundombinu rafiki bado ni kikwazo kikubwa.
Na kama taifa linaamini hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma, basi uwekezaji katika huduma hizi si hiari ni wajibu.Kwa sababu nyuma ya kila takwimu kuna mtoto kama Ayubu, na nyuma ya kila mtoto kuna ndoto inayosubiri nafasi ya kufanikiwa.





)

More Stories
Salome:Ushirikiano wa wadau ni muhimu kufikia lengo la Nishati Safi ya Kupikia
Wazalishaji teknolojia nishati safi watakiwa kufuata viwango
Mgawanyo wa hisa NMB wafungua mlango kwa wawekezaji wapya