Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga
HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC, imeanza ujenzi wa kitengo maalumu cha matibabu ya magonjwa ya moyo ambacho kinatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),kufuata matibabu ya kibingwa ya ugonjwa huo.
Hatua hiyo imekuja wakati mahitaji ya huduma za matibabu ya moyo yakiendelea kuongezeka nchini Tanzaniahuku asilimia 70 ya wagonjwa kutoka ukanda wa Kaskazini wameshindwa kupata huduma za kibingwa za ugonjwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),kutokana na changamoto za gharama kubwa za usafiri pamoja na malazi.Hali inayochangia baadhi kuchelewa kupata matibabu au kushindwa kabisa kufika kwenye vituo vya huduma.
Hata hivyo kitengo hicho kinatarajiwa kuhudumia kati ya asilimia 40 hadi 60 ya wagonjwa wa moyo kutoka mikoa ya ukanda huo.
Akizungumza jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian,amesema ujenzi wa hospitali hiyo ni mkombozi kwa wananchi wa ukanda wa Kaskazini,na tayari jitihada mbalimbali zinaendelea kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara, taasisi binafsi,mashirika pamoja na wananchi,kujitokeza kuchangia fedha kwa ajili ya kuendeleza mradi huo huku lengo kubwa likiwa ni kukusanya zaidi ya sh.bilioni 3,kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali hiyo ya kisasa ya moyo.
“Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa inayohudumiwa na hospitali ya KCMC, hivyo uwepo wa kitengo hiki utaondoa adha kubwa kwa wananchi wetu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda jijini Dar-es -Salaam kutafuta huduma za moyo,”amesema Balozi Dkt. Burian.
Kwa upande wake Meneja wa Miradi na Ofisa Mipango wa Hospitali ya KCMC ambaye pia ni Mratibu wa ujenzi wa kitengo cha magonjwa ya moyo, Emmanuel Bianchi,amesema mradi huo tayari umefikia asilimia 40 ya utekelezaji wake.
Ambapo gharama halisi za mradi huo ni sh.bilioni 25 ambapo tayari wamefanikiwa kupata msaada wa zaidi ya sh.bilioni 22 kutoka kwa wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi huku kiasi kilichobaki cha sh.bilioni 3 kinahitajika kukamilisha ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.
“Kimsingi huu ni mradi mkubwa unaolenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya za kibingwa na kibingwa bobezi hapa nchini. Tunataka kuhakikisha wananchi wa ukanda wa Kaskazini wanapata huduma bora karibu yao bila kulazimika kwenda mbali,”amesema Bianchi.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa kitengo hicho kutasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda JKCI jijini Dar-es -Salaam pamoja na idadi ya wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu ya moyo jambo ambalo limekuwa likitumia fedha nyingi za wananchi na Serikali.
Aidha amesema wagonjwa wengi waliokuwa wakipewa rufaa kwenda JKCI, wamekuwa wakikwama kutokana na mazingira ya jiji la Dar-es-Salaam ikiwemo gharama za usafiri, malazi na maisha ya kila siku, hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kabisa kufika kupata huduma kwa wakati.
“Huduma hizi kusogezwa karibu na wananchi ni hatua kubwa ya kuokoa maisha ya watu wengi pamoja na kupunguza mateso kwa familia ambazo zimekuwa zikigharamia safari za muda mrefu kutafuta matibabu,”.

More Stories
Takukuru yageukia utapeli kwenye makundi ya WhatsApp
TPTC yazindua awamu ya pili,Kozi ya wanawake masuala ya Ulinzi na Usalama
Wanawake wahimizwa kugombea nafasi mbalimbali