Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga
ZAIDI ya wakazi 27,000 katika kata za Ngogwa na Kitwana wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga wanatarajia kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji wa Ngogwa – Kitwana unaotarajiwa kufunguliwa rasmi mwezi Oktoba, 2021.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi mjini Kahama na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Shinyanga (SHUWASA), Mwamvua Jilumbi kukamilika kwa mradi huo kutamaliza tatizo la muda mrefu la ukosefu wa maji kwa wakazi wa kata hizo mbili.
Jilumbi ambaye Mamlaka yake ndiyo inayotekeleza mradi huo amesema kinachosubiriwa kwa sasa ni shughuli za ufungaji wa bomba kutoka bomba kuu linalotoa maji Shinyanga kwenda kwenye tangi kubwa lenye ujazo wa lita za ujazo 8,000 lilipo kwenye kilima cha Ngogwa.
Hata hivyo mwenyekiti huyo amesema mradi huo ulitakuwa kukamilika mwishoni mwaka 2020 lakini palitokea tatizo la mzabuni aliyepewa kazi ya kupeleka mabomba ya plastiki badala ya mabomba ya chuma kinyume na mkataba wake hivyo kuchelewesha kukamilika kwa mradi kwa wakati.
“Mradi huu ulipaswa uwe umekamilika mwishoni mwa mwaka 2020, lakini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa upatikanaji wa mabomba ya chuma ambayo kwa kiasi kikubwa ilisababishwa na mzabuni aliyepewa kazi ya kutuletea mabomba,”
“Mzabuni huyo alitakiwa kutuletea mabomba ya chuma kwa mujibu wa maelekezo yaliyomo ndani ya mkataba, yeye alituletea ya plastiki, baada ya mazungumzo ilibidi Mamlaka tuvunje mkataba na mzabuni huyo na kutafuta mtu mwingine, ambaye yupo mbioni kutuletea mabomba yanayotakiwa, wakati wowote mabomba hayo yatawasili,” ameeleza Jilumbi.
Jilumbi amesema matarajio yao ni kwamba kazi zote zitakamilika ndani ya kipindi kifupi kuanzia hivi sasa na itakapofika mwezi Oktoba mradi huo utakuwa umekamilika wote na wananchi watarajie kuanza kupata maji safi na salama.
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa kutokana na changamoto zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa mradi huo wamejifunza mambo mengi ambapo tayari wamewaelekeza watendaji ndani SHUWASA kuhakikisha wanakuwa makini kila pale wanapoingia mikataba na wazabuni kwa ajili ya kuwaletea vifaa mbalimbali.
“Ni kweli tumejifunza mambo mengi kutokana na changamoto zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa mradi huu, tumepata fundisho, na tumesema kuanzia sasa watendaji wetu kabla ya kupokea vifaa vinavyoletwa wawe makini kwa kuangalia iwapo ndivyo vinavyohitaji na vina ubora unaotakiwa, hii itatusaidia tusikwame tena,” ameeleza Jilumbi.
Katika maelezo yake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola amesema mradi wa Ngogwa – Kitwana unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 2.4 kutokana na kutekelezwa na wataalam wa ndani (force account) na mpaka sasa serikali imeishatoa kiasi shilingi bilioni 2.2 na kazi zinazoendelea zipo katika hatua ya mwisho.
“Mradi huu unatarajiwa kunufaisha wananchi 27,000 wanaoishi katika kata za Ngogwa na Kitwana, na hapo awali ulitarajiwa kutekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4 iwapo ungetekelezwa kwa kutumia mkandarasi, lakini baada ya kuagizwa tutumie wataalam wa ndani, tutatumia shingili bilioni 2.4.,” ameeleza Mhandisi Katopola.
Baadhi ya wakazi wa kata za Ngogwa na Kitwana wakiwemo wanafunzi na walimu wa shule ya msingi Ngogwa wilayani Kahama wameipongeza Serikali kwa kuwapelekea mradi huo wa maji na kwamba hivi sasa wataondokana na changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama katika maeneo yao.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea mradi huu wa maji, utatupunguzia kwa kiasi kikubwa usumbufu wa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwa ajili matumizi yetu ya kila siku, hasa sisi wanafunzi, maana tulikuwa tunapitwa baadhi ya masomo kwa ajili ya kufuata maji, kwa sasa shida hii itaisha,” ameeleza mwanafunzi Marco Paschal.
Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Shinyanga (SHUWASA) walikuwa na ziara ya siku moja ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa maji wa Ngogwa – Kitwana wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga, ambapo mara baada ya kukamilika kwake utakabidhiwa kwa Mamlaka ya Maji – Kahama (KUWASA) kwa ajili ya uendeshaji wake.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi