April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kasi ya wataalamu wa Bima nchini yatarajia kuongezeka.

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

SERIKALI imesema kuanzishwa kwa mtaala wa Bima na Wanagenzi itakuwa sehemu ya ongezeko la wataalamu wa bima nchini ambao watakuwa sehemu ya utatuzi  wa Changamoto mbalimbali zinazowakumba wananchi katika  sekta hiyo.

Pia imesema  imejidhatiti katika kuimarisha sekta ya bima nchini kwa kuweka mipango Madhubuti ya kuendeleza soko la bima ambapo kwa kiasi kikubwa  imerejesha imani  kwa wananchi juu ya bima zinazotolewa.

Akizungumza hayo jana mkoani Dar es Salaam,wakati wa uzinduzi wa Mtaala wa Bima na Wanagenzi unaotolewa na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA)kwa kushirikiana na Shirika la Bima Tanzania(NIC), Mkurugenzi wa Ukaguzi  na Usimamizi  wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA)Neema Lutula,  amesema kupitia jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa kiasi kikubwa itachangia makampuni  ya bima yaliyosajiliwa nchini kuongeza ajira kwa vijana wakitanzania ambao wana uweledi wa masuala ya bima watakaohitimu katika Chuo hicho.

“Mamlaka ya bima nchini itaendelea kutoa ushirikiano kwa Chuo pamoja na NIC, muda wowote ili kuhakikisha azma ya kuanzisha mtaala huu unafanikiwa kwa asilimia 100,”alisema na kuongeza

“Kuanzishwa kwa mtaala huo itakuwa chachu ya kuendelea  kutoa wataalamu bora kwa Chuo cha Uhasibu Arusha hivyo natoa rai kwa watanzania kuendelea kutumia bima zinazotolewa na makampuni mbalimbali ya bima,”amesema

Amesema watanzania nchini hususani wenye  sifa ya kusoma stashada ya Bima na wanafunzi katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) wachangamkie  fursa hiyo ili kuongeza wingi wa wataalamu wa masuala ya bima na wanagenzi  wenye uweledi wa kutosha.

Amesema wataalamu  hao watasaidia jamii kunufaika na uwepo wa sekta ya Bima katika uchumi na maisha yao ya kila siku ,hususani katika kupata elimu ya kinga na majanga mbalimbali kiuchumi na kijamii.

Aidha amesema  sekta ya bima inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo muamko mdogo wa wananchi kununua bima,huduma kuwafikia wananchi  hususani wa vijijini na elimu ndogo masuala ya bima kuhusu bidhaa tofauti tofauti.

“Kuanzishwa kwa mtaala huu utakuwa ni sehemu ya hitimisho ya upungufu wa wataalamu wa Bima ambao watakuwa sehemu ya uteuzi wa changamoto  hizo ,”amesema na kuongeza

“Mamlaka ya usimamizi wa bima kama mdau muhimu tunaamini kwamba wataalamu watakaondaliwa watakuwa wanapanua wigo wa usambazaji wa huduma ya bima kwa wananchi ,uandaji  wa bidhaa yakidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza idadi ya Makampuni yanayotoa huduma za Bima, “amesema Lutula

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha,Prof.Eliamani Sedoyeka akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa mtaala mpya wa kozi ya Bima na wanagenzi itakayotolewa katika chuo hicho.

Kwa Upande wake Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha , Profesa Eliamani Sedoyeka amesema  kama chuo wapo tayari kuwasaidia kwa chochote wanafunzi hao watakachohitaji pindi watakapomaliza elimu yao.

Amewataka wahitimu hao , kutumia muda  wanaokuwa  chuoni kuanza kufikilia namna ya kujiajiri wenyewe na baadae kuja kuajili wenzao.

“Katika sekta ya bima mtakapoingia mjitume,muanze kuhakikisha mnatoa mchango katika kampuni na kujifunza na wewe utapomaliza uanze kujitegemea,”amesema na kuongeza

“Wanafunzi hawa tayari wamesoma semiter mbili kuanzia mwezi huu mwishoni wanaenda NIC watakaa  miezi 14 kwa muajili   na miezi 14 chuoni,”amesema

Naye Mkurugenzi wa NIC,Dkt. Elirehema Dorie amesema  wao kama Shirika wanawapokea wanafunzi hao na kuwaandaa kuwa wahitimu kamili ambapo wanapotaka katika Shirika lao wanakuwa wamejifunza kikamilifu.

“Tunapompokea mwanafunzi lazima afate maelekezo atakayopatiwa akiwa kwenye kazi tunahakikisha tunamuandaa mtu kamili ili anapotoka Chuo anaenda moja kwa moja katika ajira,”amesema  Dorie