April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Karakana na Mifumo ya Chuo cha Bahari Dar es salaam kuboreshwa kutoa fursa ya mafunzo Online

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

CHUO cha Bahari Dar es salaam (DMI)  kimesema kinampango wa kuboresha karakana ya mafunzo kwa kuongeza vifaa na maeneo ya kujifunzia kuwa ya kisasa zaidi ili kuendana na mabadaliko ya sayansi na teknolojia pamoja na soko la ajira.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Februari 9,2023 na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho ,Dkt.Tumaini Gurumo  wakati akizungumza na waandishi wa habari kueleza utekelezaji wa majukumu ambapo amesema ujenzi na ukarabati wa mifumo ya Tehama itasaidia kutoa fursa ya mafunzo kwa masafa marefu(Online) ili kuzalisha mabaharia wenye kuendana na teknolojia za sasa.

Dkt.Gurumo amesema kuwa maboresho hayo ya karakana yatasaidia wanafunzi wao kutokuwa wageni wa vifaa  wanayokutana navyo wanapokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo.

Aidha amesema kuwa DMI imeanza utaratibu wa kujenga uhusiano na wamiliki wa meli ili kupata nafasi za ajira na mafunzo kwa vitendo kwa ajili ya mabaharia wa kitanzania nje na ndani ya nchi.

“Tayari DMI imefanikiwa kuwaunganisha na waajiri mabaharia 27 na kufanikiwa  kupata ajira na mafunzo kwa vitendo,”amesema Dkt.Gurumo.

Pamoja na hayo Dkt.Gurumo ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita imewezesha kupata maeneo mbalimbali ya kujenga matawi ya DMI katika Mikoa ya Lindi na Mwanza.

“Matawi haya yatakapo kamilika huduma ya elimu na mafunzo ya usalama wa vyombo vya usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji itakuwa imesogezwa karibu zaidi na wananchi,”amesema.

Amesema kuwa matawi hayo yatawezesha vijana wengi zaidi kupata elimu na kupanua wigo wa ajira kwasababu soko la ajira ya ubaharia nchini linaendelea kuongezeka na katika ulimwengu ni kubwa kwasasa.

Vilevile amezungumzia mipango mingine ya Chuo hicho kuwa ni pamoja na kujenga vyombo vidogo vidogo vya usafiri majini ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo,kujenga miundombinu ya chuo kwa viwango vya juu mkabala na ufukwe wa bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam ilikukidhi mahitaji ya ongezeko la wanafunzi,walimu na kozi.

Pamoja na kupeleka elimu na mafunzo ya ubaharia katika maendeleo mengi zaidi ya nchi yetu ikiwemo Pemba na Kigoma.