May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kanisa laomba msaada wa Rais Samia Arusha

*Ni baada ya waumini kukuta limezungushiwa uzio wa mabati, kufuatia mgogoro wa ardhia, wadai wameporwa haki ya kuabudu

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline, Arusha

WAUMINI wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) la jijini Arusha, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati mgogoro wa ardhi uliopelekea kushindwa kusalia ndani ya kanisa lao na badala yake ibada imefanyikia nje ya nyumba ya mtu.

Waumini wa Kanisa hilo la KKAM lililopo Ngulelo Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, wamefikia hatua hiyo jana baada ya kufika kwenye kanisa lao kwa ajili ya ibada, lakini walipigwa butwaa baada ya kukuta limezungushiwa uzio wa mabati.

Kwa mujibu wa habari kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika, uzio huo wa mabati unadaiwa kuzungushwa na mtu anayedai ni mmiliki wa eneo hilo baada ya kushinda kesi.

Kwa mujibu wa watoa taarifa eneo la kanisa hilo lilizungushiwa mabati wiki iliyopita na mtu anayetajwa kuwa mmiliki wa eneo hilo, baada ya kushinda kesi ya madai ya kuvamiwa eneo la familia yake na kuendelezwa bila kibali cha familia.

Habari za ndani, zimeelezwa kwamba katika shauri hilo, Askofu wa Kanisa hilo la KKAM, Philemon Mollel (Monaban) ndiye aliyedaiwa kuvamia eneo hilo na kujenga kanisa lililokuwa linatumiwa na waumini hao, kabla ya jana kukuta limezungushiwa uzio wa mabati.

Hata hivyo, waumini waliozungumza na wanahabari jana, walimuomba Rais Samia, awasaidia kwani kitendo cha kanisa lao kuzungushiwa uzio ni kuporwa uhuru wa kumtukuza Mungu.

“Kuabudu ni haki ambayo tumepewa na Katiba, sasa kitendo cha mtu huyu kujenga uzio ni uporaji wa haki yetu, ndiyo maana tunamuomba Rais Samia atusaidie,” alisema mmoja wa waumini kwa jaziba.

Amedai eneo hilo ni lao hivyo wanamuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati mgogoro huo.

Amesema mgogoro huo hawajawahi kuusikia zaidi ya juzi kukuta eneo la kanisa limezungushiwa mabati na kufuli kubwa kila pembe, hivyo vipindi vya ibada na mafundisho kushindwa kufanyika.

Aidha, waumini hao walimuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na Rais Samia kupata eneo mbadala kwa ajili ya kuendesha ibada wakati mgogoro huo ukitafutiwa ufumbuzi zaidi.

“Tunaomba viongozi wetu watusaidie hasa Rais wetu Mama Samia aone hilo jambo ni la Kimungu zaidi atupatie eneo lingine la kusalia, kwani tunataabika na watoto tunaowalea kiroho wanateseka.

Mchungaji wa kanisa hilo, Emmanuel Mollel, amesema baada ya kukosa pa kusalia na waumini wamefika, wameamua kufanya ibada nje ya nyumba ya mmoja wa viongozi wa kanisa hilo.

“Ibada ni kila kitu kwenye huu ulimwengu, hivyo baada ya kukuta kanisa limefungwa na bahati mbaya waumini wote hawakupata taarifa, walilazimika kufanya ibada hapa nje tukiendelea na maombi kwa viongozi wetu wa Serikali waangalie jambo hili upya, lakini pia kutupatia eneo mbadala la kusalia,” alisema Mchungaji Emmanuel.

Ka upande wake, Askofu Monaban alisema hali hiyo imetokea baada ya Mahakama kumpatia ushindi aliyemshtaki kwa madai alivamia eneo hilo.

“Eneo hilo nilinunua mwaka 2009 kwa Jimmy Titus Mollel, ambaye alikuwa msimamizi wa mirathi ya mali ya baba yake, Titus Mollel.

Alidai wamekubaliana na familia anayoisimamia kuuza. Alisema eneo hilo la kanisa, kiwanja namba 31, kikiwa pamoja na viwanja namba 29, 30 na 32 vyote kwa pamoja, vina ukubwa wa ekari mbili alivyonunua sh. milioni 360 milioni.

Amesema maeneo hayo hajayavamia, ameyanunua kihalali na kuwekeza kituo cha mafuta, sehemu ya kuoshea magari, kanisa na supamaketi, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh. bilioni 2.5.

Alisema anashangaa Mahakama kutoa hukumu ya kuamuru arudishe ardhi ya watu bila kujali kuwa nimewekeza na nirudishiwe fedha zake.

Alisema anatarajia kukataa rufaa dhidi ya shauri hilo, hivyo kuwataka watu wanaotaka kununua maeneo hayo wasikubali kwani bado kuna mgogoro.

Kwa upande wake, mmoja wa wanafamilia wanaodai eneo lao, William Mollel, alisema wameamua kuzuia shughuli zozote kuendelea katika eneo lao lililovamiwa.

“Baba yetu alituchia hili eneo sisi familia yake, na Monaban alikuja kumrubuni aliyekuwa msimamizi wetu wa mirathi akadai amenunua,” amesema.