July 31, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kange kuunga mkono ujenzi wa barabara

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

WANANCHI wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki,Kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela mkoani Mwanza wameanza ujenzi wa barabara ya Sinza-Mjimwema yenye urefu wa kilomita 0.5 kwa kiwango cha zege kupitia michango ya kila kaya kutoa mfuko mmoja wa saruji.Ujenzi huo ni awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza kutekelezwa mwaka jana.

Baada ya kuanza kwa ujenzi huo, Diwani wa Kata ya Nyamanoro,Abdulrahman Kange,amewapongeza wananchi kwa hatua hiyo huku akiahidi kuungana nao katika jitihada hizo ili kuhakikisha lengo la kuwa na miundombinu bora inayopitika linatimia.

Akizungumza Julai 30,2026 na Timesmajira kwa njia ya simu Kange amesema,alitembelea maeneo hayo na kujionea namna wananchi wanavyounga mkono utekelezaji wa maendeleo katika miundombinu, hivyo naye ataendelea kuunga mkono kwa namna moja au nyingine kuhakikisha miundombinu rafiki inapatikana kwa wakazi wa maeneo hayo.

Amesema kutokana na jiografia ya Kata ya Nyamanoro changamoto za miundombinu ni kubwa, hivyo kwa kuwa mwaka wa fedha umeanza, lengo ni kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote kwa kiwango cha kawaida na baadaye kwa kiwango cha lami au zege,hivyo wameandika maandiko na kuomba Halmashauri kufanikisha miradi hiyo ambayo wananchi wamekuwa wakiihitaji kwa muda mrefu.

Kange amesema wananchi wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki walikubaliana kila kaya kununua mfuko mmoja wa saruji kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha zege na zoezi lilianza Jumamosi iliyopita ya Julai 25,2026,huku katika mtaa mwingine aliunga mkono ujenzi wa barabara kwa kutoa mifuko mitano ya saruji.

“Nawapongeza wananchi wa mtaa huu kwa hatua hii,tumekubaliana kuwa Jumamosi, Agosti 1, 2026, tutaenda hatua ya pili ya ujenzi wa barabara na mimi kama Diwani ninaunga mkono kulingana na mazingira na kadri ninavyohitajika,tutafika na kushirikiana pamoja kuhakikisha barabara hiyo inapitika,”amesema Kange.

Hata hivyo amewahimiza wananchi wa mtaa huo ambao bado hawajatoa mfuko wa saruji kutekeleza makubaliano ya kila nyumba kutoa angalau mfuko mmoja,ambapo alisema barabara hiyo ikikamilika itaongeza thamani ya maeneo yao, kurahisisha usafiri na upatikanaji wa huduma muhimu, ikiwemo magari kuwafikia wagonjwa kwa urahisi pamoja na kurahisisha wananchi kufika nyumbani kwa usalama nyakati za usiku.

Aidha,amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali na viongozi katika kuunga mkono shughuli za maendeleo badala ya kuiachia Serikali pekee huku akisisitiza viongozi wanaendelea kutoa elimu kupitia mikutano kuhusu usafi wa mazingira ili kusaidia barabara zisiweze kuharibika kutokana na kuziba kwa mitaro na kushindwa kupitisha maji.

Itakumbukwa kuwa wakati akizungumza na Majira wakati wa zoezi la wananchi kufanya usafi na kupanga mawe eneo korofi la barabara hiyo ambayo ilikuwa hatua ya awali kabla ya kuanza zoezi la kumwaga zege, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki Missa Budundu,alisema barabara hiyo inategemewa na wananchi zaidi ya 4,000 wa mtaa huo pamoja na mitaa ya Kata jirani ya Nyasaka.

Ambapo ametoa ombi kwa Serikali na wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi hizo ili barabara hiyo iweze kukamilika kwa haraka na ubora ili ipitike kwa urahisi wakati wote.

Amesema zoezi hilo ni muendelezo wa utekekalezaji wa kujenga barabara ulioanza mwaka jan,hivyo katika kikao cha robo mwaka cha mtaa huo kilichofanyika hivi karibuni walikubaliana na wananchi kuwa kila kaya itachangia mfuko mmoja wa saruji ili kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha zege.