July 31, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CAP LC yawasilisha hoja UNHRC

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la CAP LC limewasilisha taarifa ya maandishi katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), likieleza wasiwasi kuhusu kile lilichodai kuwa ni kuongezeka kwa ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya wanachama wa Shincheonji Kanisa la Yesu waliopo nje ya Korea Kusini.

Taarifa hiyo imewasilishwa wakati wa Kikao cha 62 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kuanzia Juni 15 hadi Julai 10, 2026, ikiwa ni sehemu ya ajenda ya kukuza na kulinda haki za binadamu, zikiwemo haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shincheonji Kanisa la Yesu, CAP LC imeeleza kuwa maamuzi ya kiutawala na kimahakama yanayohusu taasisi za kidini yanapaswa kufanywa kwa kuzingatia ushahidi unaoweza kuthibitishwa na si taarifa au mitazamo ambayo haijathibitishwa.

Shirika hilo limedai kuwa baadhi ya taarifa hasi kuhusu Shincheonji zilizotolewa nchini Korea Kusini zimeendelea kusambazwa katika mataifa mengine na hivyo kuathiri maoni ya umma, pamoja na maamuzi ya baadhi ya mamlaka za kiutawala na kimahakama dhidi ya wanachama wa kanisa hilo.

Kutokana na hali hiyo, CAP LC imezitaka serikali mbalimbali kuhakikisha kuwa maamuzi yoyote yanayohusu Shincheonji Kanisa la Yesu yanazingatia misingi ya sheria, haki na ushahidi, ili kulinda uhuru wa dini na kuzuia vitendo vya ubaguzi dhidi ya makundi ya kidini yaliyo wachache.

Kwa upande wake, Shincheonji Kanisa la Yesu limesema kuwasilishwa kwa taarifa hiyo mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kunaonyesha kuwa suala hilo limevuka mipaka ya Korea Kusini na sasa linapewa uzito katika majukwaa ya kimataifa yanayoshughulikia haki za binadamu.

Aidha, kanisa hilo limesema kuwa kukubalika kwa unyanyapaa usio na ushahidi kunaweza kuweka mazingira hatarishi kwa makundi mengine ya kidini yaliyo wachache duniani, na hivyo kusisitiza umuhimu wa mataifa kulinda haki za waumini wote bila ubaguzi.

CAP LC ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali lenye hadhi maalumu ya ushauri katika Baraza la Uchumi na Masuala ya Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC), ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiwasilisha masuala yanayohusu uhuru wa dini katika majukwaa ya kimataifa.

Katika taarifa yake, CAP LC pia imetaja mifano kutoka Uingereza na baadhi ya nchi zinazozungumza Kijerumani, ikidai kuwa wanachama wa Shincheonji wamekuwa wakikumbana na changamoto za kijamii na kiutawala kutokana na taarifa hasi zinazowahusu, hali ambayo shirika hilo linasema inapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria.