December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni za simu zatakiwa kubuni teknolojia yenye gharama nafuu

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Makampuni ya simu kubuni teknolojia ya gharama nafuu itakayowezesha kila Mtanzania kupata huduma ya Mawasiliano popote alipo nchini.

Rais Samia amesema hayo jijini hapa leo,Mei 13,2023 wakati wa utiaji saini mikataba ya upelekaji huduma za mawasiliano nchini kati mfuko wa mawasiliano kwa wote(UCSAF) na watoa huduma za mawasiliano ambapo minara simu 758 inakwenda kujengwa vijiji na minara 304 inaenda kuongezewa uwezo nchini.

Aidha ameyata Makampuni hayo kuleta teknolojia inayoendana na mazingira ya Tanzania kwa kuwa zipo changamoto zinazotokana na hali ya kijiografia na kipato kidogo cha wananchi katika baadhi ya maeneo.

Pia amewataka Wakala wa Barabara mijini na Vijiji (TARURA)Kushirikiana na UCSAF na wakandarasi kuhakikisha njia zinapitika katika maeneo ya vijijini inapokwenda kujengwa minara hiyo.

“Huko miaka ya nyuma UCSAF mlikuwa mnajenga minara 30 wakati mwingine 50 lakini sasa mnatarajia kujenga minara zaidi ya 700 sio kazi ndogo, lazima Rais niwepo katika kushuhudia mikataba ikisainiwa,

“Nimetoa pongezi nyingi kwa utekelezaji wa mradi huu kwa vile sasa mikoa yote 26 ya Tanzania bara inakwenda kupata huduma bora za mawasiliano baada ya Zanzibar kufikiwa na huduma hii mwezi Novemba, 2022,

“Huu ni utekelezaji mzuri wa ahadi niliyokuwa nikitoa mara kadhaa napokutana na wananchi niliahidi kukuza na kuimarisha Sekta ya TEHAMA ili kutoa ajira kwa vijana na kusukuma maendeleo ambapo mradi huu ni utekelezaji mmoja wapo wa ahadi hiyo,”amesema Rais Samia.

Amesema kuwa kuwepo kwa huduma bora za mawasiliano, hususani katika maeneo ya vijijini, ni muhimu sana kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiutamaduni na hata katika masuala ya ulinzi na usalama kwa nchi.

“Tulichokishuhudia leo ni kichocheo kikubwa cha mafanikio kwani huwezesha sekta zote kukua,

“Tutamaliza kadhia ya mawasiliano vijijini, tunakwenda kukuza biashara na kutafuta soko kwa uhakika kila mmoja awe Mkulima, Mwalimu na wananchi wote waliopo Vijijini watakuwa na taarifa kwenye viganja vyao,”amesema.

Ameeleza kuwa jambo kubwa zaidi ni badilisha teknolojia vijijini, kwa sasa hivi wakulima wana simu maarufu kwa jina la ‘vitochi’ lakini mitandao itakapoimarushwa upatikanaji wa huduma za mawasiliano, wakulima watatoka kwenye tochi kwenda kwenye tachi.

“Simu za tachi ndizo zitakazowapa taarifa zote za nchi na za Dunia, kwa hiyo tunakwenda kupeleka ukuaji wa teknolojia kule vijijini na moja ya huduma za mawasiliano zinayofanywa na UCSAF, ni kuimarisha huduma za matibabu mtandao ‘Telemedicine’ kwenda vijijini, huduma hizi zitatusaidia kupunguza vifo vya mama na watoto wakati wa kujifungua,

“Tunachokifanya leo, kinagusa sekta mbalimbali za nchi yetu, tutakuza maendeleo mijini na vijijini ili wote twende kwa kasi, si jambo dogo ni kubwa sana ndio maana nimesema niwepo ili nishuhudie,”amesema.

Amesema kuw fedha zinazotolewa ni ruzuku kutoka Serikalini, lakini kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 26.36 ambazo ni sawa na fedha za kitanzania Shilingi bilioni 60.7, ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na Shilingi bilioni 70.16 zinatokana na tozo zinazolipwa na makampuni ya simu kwa Mfuko wa UCSAF

“Miradi hii ya ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi, inatoa msukumo mzuri wa maendeleo, hivyo nawaomba sekta nyingine ziige mfano huo na Utekelezaji wa mradi huu ni hatua muhimu sana katika kuelekea Mapinduzi ya Nne ya Maendeleo ya Viwanda ambayo msingi wake ni kufikia uchumi wa kidijiti unaoifanya Sekta ya Mawasiliano kuwa nyenzo wezeshi kwa maendeleo ya sekta zote ndani ya nchi yetu,

“Kukamilika kwa mradi huu, kutasaidia sana kukuza Pato la Taifa kutokana na kuongezeka kwa wigo wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na Mawasiliano katika sekta nyingine,”amesema

Akizungumza katika hafla hiyo Mtendaji Mkuu wa UCSAF Justina Mashiba amesema katika kuhakikisha wanafikisha huduma ya mawasiliano vijijini wanaenda kujenga minara 758 katika kata 713.

Amefafanua kuwa katika minara hiyo Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) walishinda zabuni katika kata 104 na watajenga minara 104, Vodacom Tanzania amelishinda kata 190 watajenga minara 190, Airtel Tanzania walishinda kata 161 na watajenga minara 168 , Tigo walishinda zabuni katika kata 244 na watajenga minara 262 na Haloteli walishinda zabuni katika kata 34 na watajenga minara 34.

Aidha amesema pia katika mkataba huo wanaenda kuongea nguvu katika minara 304 ambayo ilikuwa inatoa huduma ya 2G sasa itaanza kutoa huduma kwa 3G na maeneo mengine 4G.

“Lengo kubwa la kuanzisha UCSAF ni kupeleka mawasiliano maeneo ya vijijini na kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya mawasiliano bila vikwazo ambapo katika kuhakikisha hilo hadi sasa tumeshajenga minara nchi nzima ,

”USCAF Imepeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za umma ambapo hadi sasa tumepeleka katika shule 4750.pia tunaendelea na mradi wa tiba mtandao lengo ni kuhakikisha watanzania wanapata huduma bila kwenda Hospitali,”amesema

Justina alifafanua kuwa lengo la mfuko ni kuhakikisha wanafikisha mawasiliano mipakani na katika mbuga za wanyama pia.