March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Masuala ya Umma na Mawasiliano wa Kampuni ya Coca-Cola Kwanza,Haji Ally Mzee(kushoto) akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani).

Kampeni ya mchanga pekee yabaini wingi wa utupwaji wa chupa za plastiki pembezoni mwa fukwe

Na Mwandishi wetu,TimesMajira,Online

IMEELEZWA kuwa  kupitia Kampeni ya Mchanga Pekee inayofanya usafi pembezoni mwa eneo la bahari hususani katika fukwe ya  Coco,imebaini kuwepo kwa  idadi kubwa ya vipande vya chupa za plastiki ,  pini, sindano, vifuniko vya chakula, majani, vifungio vya plastiki, mifuko ya kubeba plastiki pamoja na makombo ya chakula kutoka kwenye takataka .

Uchafu huo unatokana na jamii kutokuwa makini katika utunzaji wa mazingira na badala yake kutupa ovyo takataka  pasipokuweka katika vyombo maalum vya kuhifadhia taka.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masuala ya Umma na Mawasiliano wa Kampuni ya Coca-Cola Kwanza,Haji Ally Mzee ,amesema asilimia kubwa ya taka za baharini zinatoka pwani kupitia mito , mifereji ya maji na fukwe ambapo inakadiriwa kuwa kila kilomita ya mraba ya bahari ina vipande 13,000 vya vifaa vya taka za plastiki.

Amesema kila mwishoni mwa wiki, fukwe hiyo ya Coco  hupokea wastani wa watu 300 hadi 500 kwa nyakati tofauti ambapo wamekuwa wakiwasisitiza na kuwakumbusha uhifadhi mazingira kwa mustakabali wao na vizazi vijavyo.

“Hivi sasa, zaidi ya watu 5,000 wanaokuja katika maeneo hayo wameelimika na kufanikiwa kutumia vyombo maalum vya taka, kutupa taka baada ya matumizi,”amesema na kuongeza

“Kupitia kikundi chao  cha kusafisha pwani, makadirio ya chupa za plastiki 150, zaidi ya vifungashio 250 vya plastiki ni idadi kubwa ya uchafu wa baharini ambao ulihamia pwani na mawimbi yenye nguvu ya bahari zilikusanywa,”amesema

Mzee amesema chupa za plastiki zinazokusanywa  husafirishwa moja kwa moja kwa wazalishaji wa chupa za plastiki kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa za plastiki nyingine.