May 13, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi nchini kupokea daftari za Samia bure

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online,Dar es Salaam

KAMPENI ya ” Daftari la Mama” yenye lengo la kugawa madaftari bure kwa wanafunzi wa shule zote nchini, imezinduliwa leo jijini Dar es Salaam na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Yoge.

Akiongea na Waandishi wa Habari katika uzinduzi wa Kampeni hiyo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere, amesema uzinduzi wa kampeni hiyo ni muendelezo wa juhudi za taasisi hiyo ikiwa na lengo la kusaidia wanafunzi wote nchini.

Nyerere amesema, ugawaji wa daftari hizo huku kila daftari moja likiwa na kurasa 200 kwa wanafunzi, utasaidia kuwapunguzia mzigo wazazi hususan ambao hawana uwezo wa kujikimu kuwanunulia madaftari watoto wao pindi wanapokuwa na uhitaji.

” Kama mnavyokumbuka mwaka jana tulikuwa na kampeni ya Samia nivishe viatu,lakini tukafikiria mbali zaidi kuwa mtoto huyu amevishwa viatu, lakini anaweza akawa hana daftari la kuandikia masomo yake hivyo mama akaona ni bora atoe madaftari bure kwa wanafunzi nchi nzima,”amesema Nyerere.

Amesema zoezi hilo la ugawaji wa daftari kwa wanafunzi litafanyika Tanzania Bara na Zanzibar na kudai kuwa hivi sasa wapo katika mchakato wa kuangalia Mkoa upi utakaoanza kupokea daftari hizo.

Anaongeza kuwa, daftari hizo zipo za aina mbili, ambapo zipo za mama zenye picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na daftari la baba, lenye picha ya Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi.

Aidha kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali Yoge, Philomena Mwalongo, anadai wao kama wadau wameona ni vyema wakaunga mkono juhudi za Rais Samia, katika kuhakikisha anamuinua mwanafunzi kielimu.

” Sisi kama Yoge tumejikita katika mambo makuu manne ikiwemo elimu, usawa wa kijinsia, demokrasia na mabadiliko ya tabianchi hivyo kupitia suala hili tuliona ni vyema tukaunga mkono juhudi za mama anazoonesha katika kuhakikisha anamuinua mwanafunzi kielimu,”.