January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya lishe yasisitiza utoaji chakula shuleni

Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

Wajumbe wa Kamati ya Lishe Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,wamesisitiza juhudi zaidi zifanyike za kuhakikisha shule zote zinatekeleza mpango wa chakula shuleni.

Hayo yamebainishwa wakati Kamati ya Lishe ya halmashauri hiyo iliopo kutana na kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Wajumbe hao wamesema kuwa mbali na hayo pia kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhusu utoaji wa chakula katika shule zote za msingi na sekondari kwa kuhakikisha unafanyika.

Pia kuhakikisha kuwa chakula kinachotolewa kiwe ni kile kilichoongezwa virutubishi ili kuboresha afya za wanafunzi.

Awali kupitia kamati hiyo ya lishe, iliwasilishwa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa chakula shuleni ambapo Mkuu wa Divisheni ya Elimu Msingi na Awali Mwalimu Busungu, akiwasilisha taarifa ya utoaji chakula kwa shule za msingi Ilemela amesema kuwa hadi kipindi hiki jumla ya shule 52 kati ya 76 za serikali zimeanza kutoa lishe shuleni.

Hivyo ameahidi kuwa hadi kufikia mwisho wa mwezi wa Mei shule zote zitatoa lishe,kwa upande wa elimu sekondari Mwalimu Sylvester Mrimi amesema kuwa jumla ya shule 10 kati ya 32 za serikali zinatoa chakula.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe,Ofisa Lishe Paulina Machango, ameainisha shughuli mbalimbali ambazo zimetekelezwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/2023 Januari-Machi.

Baadhi ya shughuli ni pamoja na kutoa elimu ya lishe kwa wazazi/walezi katika Kata tatu za Nyamh’ongolo, Bugogwa na Ilemela, usimamizi shirikishi pamoja na uhakiki wa ubora wa takwimu za viashiria vya lishe kwa vituo vya kutolea huduma za afya ya mama na mtoto.

Ununuzi wa chakula dawa kwa ajili ya kutibu watoto wenye umri chini ya miaka 5 wenye utapiamlo pamoja na shughuli nyingine.

Taarifa juu ya kadi alama ya lishe ikiwa na viashiria 12 ambavyo vinatumika kufuatilia utekelezaji wa afua za lishe iliwasilishwa ambapo wajumbe kwa pamoja walikubaliana kuwa nguvu zaidi iongezwe katika utoaji elimu ya lishe kwa jamii ya Ilemela.

Sanjari na hayo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia Idara ya Afya imetenga kiasi cha milioni 85.8 kutoka mapato ya ndani,kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za lishe.

Hii ni kulingana na idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kwa ajili ya kutekeleza shughuli za lishe na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 77.5