November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge ya Viwanda, TCCIA kushirikiana kuchochea kukuza uchumi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

NAIBU Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameihakikishia Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kuwa Kamati ya Kudumu Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira itafanya kazi kwa karibu na chemba hiyo ili kutoa mchango stahiki ili kuchochea ukuaji wa sekta za viwanda, biashara na kilimo hapa nchini.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa ofisi ndogo ya TCCIA Makao Mkuu Dodoma, ambapo alimwakilisha Spika Job Ndugai, Dkt. Tulia alisema Chemba ina nafasi kubwa ya kutoa mchango chanya katika kukuza uchumi wa taifa na kamati ya Bunge itatoa ushikiano mkubwa.

“Sisi kama Bunge kupitia Kamati yetu ya kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira tupo tayari kushirikiana na TCCIA ilikutoa mchango chanya katika kukuza uchumi wa nchi yetu,” alisema Dkt Tulia mwishoni mwa wiki Jijini hapa,”amesema.

Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Paul Koyi (watatu kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson (katikati) ambaye alimwakilisha Spika Job Ndugai, namna Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya chemba hiyo iliyopo Jijini Dodoma itakavyotoa huduma zake kanda ya kati kwenye hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika mwishoni mwa wiki . Wapili kulia ni Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa TCCIA, Nebart Mwapwele na wakwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira, David Kihenzile.

Dkt. Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, alitumia pia fursa hiyo kuipongeza TCCIA kwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada na hatua mbalimbali zianzochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo ujenzi wa uchumi unaotegemea viwanda.

“Uzinduzi wa Ofisi hii Jiji Dodoma ambako ndiyo Makao Makuu ya nchi inaonyesha utayari wa sekta binafsi kufanya kazi kwa karibu na serikali. TCCIA ni miongoni wa taasisi za kwanza kwenye sekta binafsi kufungua ofisi hapa,”amesema.

Amesema kuwepo kwa ofisi ya chemba Dodoma kutawezesha ushiriki wake kikamilifu kwenye majadiliano na Kamati mbalimbali za Bunge hivyo kusaidia kufanya maamuzi sahihi yatakayo chochea ongezeko na ukuaji wa uwekezaji.

Dkt Tulia amesema amevutiwa na utendaji kazi wa chemba hiyo kwani imekuwa mstari wa mbele kuwawezesha sambamba na kuwapa huduma za ushauri wa namna bora ya kukuza biashara zao wajasiriamali wanawake vijana (Young Women Entrepreneurs- YWE).

Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson (katikati aliyesimama) ambaye alimwakilisha Spika Job Ndugai akizungumza kwenye hafla ya uzindua wa Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) iliyofanyika mwishoni Jijini Dodoma. Kulia ni Rais wa TCCIA, Paul Koyi na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira, David Kihenzile. Nyuma wa pili kulia Mjumbe wa Bodi ya TCCIA Dkt. Said kingu kushoto kwake ni Eutropia James na kulia kwake ni Njile Bwana.

Kwa upande wake, Rais wa TCCIA, Paul Koyi alisema uamuzi wa kufungua ofisi hiyo Jijini Dodoma unalenga kupunguza gharama wanazozitumia wanachama wake pamoja na wadau wengine kufuata huduma Dar es Salaam.

“Tumeamua kujitanua zaidi kwa kusogeza huduma karibu na wafanyabiashara wenye viwanda, biashara na kilimo kwani huwepo wa ofisi ndogo ya makao makuu kanda ya kati itashughurikia changamoto zote zinazowakabili wanachama wetu kwa haraka,” amesema Koyi.

Alisema kwa maswali mbalimbali yanayohusu kilimo viwanda na biashara wananchi wasisite kufika kwenye ofisi hiyo kwani wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanatoa huduma bora itakayo leta tija kwa wanchama.

“Naomba nitoe wito kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na mikoa ya jirani na ya kanda ya kati kuitumia ofisi ndogo ya makao makuu kushughulikia masuala ambayo yangeshughulikiwa Dar es salaam,” amesisitizi Koyi na kuongeza kuwa TCCIA ina Imani kubwa sana Bunge na Serikali ya Awamu ya Sita.

Naye Mjumbe wa Bodi ya TCCIA, Dkt. Said Mtemi Kingu amesema Chema imejimbanua kwa kutekeleza kwa vitendo azma ya serikali ya kujenga uchumi unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.

Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson (katikati) ambaye alimwakilisha Spika Job Ndugai akikata utepe kwenye hafla ya uzindua wa Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) iliyofanyika mwshoni mwa wiki Jijini Dodoma. Kulia ni Rais wa TCCIA, Paul Koyi na kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira, David Kihenzile. Picha zote na mpiga picha wetu.

“Tumekuwa mstari wa mbele katika kutoa ushauri wa namna bora ya kukuza mitaji kwa wajasiriamali, wafanyabiashara na wenye viiwanda na kilimo ili kuchochea upatikani wa ajira kupitia kazi wanazofanya na hivyo kuongeza pato la taifa.

TCCIA ni miongoni mwa taasisi chache barani Afrika zenye mtandao chini nzima ambapo mwaka 2007 ilishinda tuzo ya kuwa taasisi bora Afrika kwa kuwa na mtandao imara nchi nzima.