July 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kabudi : Banda La Waziri Mkuu lina huduma Bora

Na Joyce Kasiki,Dar

WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Profesa Palamagamba Kabudi, amewahimiza Watanzania wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu ili kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Profesa Kabudi alitoa wito huo Julai 4,2026  baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu, akieleza kuwa banda hilo ni la kipekee kwa kuwa linawakutanisha wananchi na taasisi zote tatu zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Alizitaja taasisi hizo kuwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Alisema banda hilo halitoi tu maelezo kuhusu shughuli na mafanikio ya Serikali, bali pia linashughulikia changamoto za wananchi kwa kutoa ushauri, elimu na huduma mbalimbali zinazoweza kutolewa papo hapo.

“Ninawasihi wananchi wenye changamoto mbalimbali kufika katika banda hili ili kupata ushauri na huduma zinazotolewa na wataalamu waliopo. Hapa wananchi wanapata fursa ya kusikilizwa na kusaidiwa katika masuala yaliyo ndani ya mamlaka ya Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Profesa Kabudi.

Alibainisha kuwa katika eneo la elimu, ameshuhudia vijana wengi waliomaliza kidato cha nne wakipata ushauri kuhusu uchaguzi wa tahasusi kwa wanaojiunga na kidato cha tano, huku baadhi yao wakisaidiwa kubadili tahasusi walizochagua ili ziendane na uwezo na malengo yao.

Kwa upande wa kazi na ajira, alisema wananchi wanapata huduma kutoka taasisi za hifadhi ya jamii, ikiwemo NSSF na mifuko mingine, ambapo wanapewa ushauri kuhusu usajili, mafao, pamoja na masuala yanayowahusu waliokaribia kustaafu au waliopoteza taarifa zao za uanachama.

Profesa Kabudi alisema jukumu kuu la Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu na kusimamia utendaji wa shughuli za Serikali ili kuhakikisha huduma muhimu kama afya, elimu, barabara, umeme na nyingine zinawafikia wananchi kwa ufanisi, sambamba na kuhakikisha changamoto na malalamiko yao yanapatiwa ufumbuzi.

Alieleza kuwa Maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu yanafanyika katika kipindi ambacho Serikali imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, jambo linaloyafanya kuwa ya kipekee kwa kuwa yanaonyesha mwelekeo wa maendeleo ya nchi katika miaka ijayo.

“Dira ya 2050 inalenga kujenga uchumi imara na kuboresha maisha ya Watanzania. Banda hili linaonyesha mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali tunazosimamia, zikiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara na maendeleo ya jamii,” alisema.

Aidha, alisema wafanyabiashara na wawekezaji wanaotembelea banda hilo wanaweza kupata taarifa na ushauri kuhusu fursa za uwekezaji, mikopo na huduma zinazotolewa kupitia mifumo mbalimbali ya Serikali kwa lengo la kukuza uchumi na biashara.Alisema  kuwa banda la Ofisi ya Waziri Mkuu ni sehemu muhimu ambayo wananchi wanapaswa kutembelea ili kujifunza, kupata huduma na kushuhudia hatua kubwa ya maendeleo ambayo Tanzania imeifikia, pamoja na kuelewa mwelekeo wa maendeleo ya taifa chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.