Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Tanga
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wabunifu, wavumbuzi na wataalamu mbalimbali nchini kusajili ubunifu na kazi zao ili kupata haki ya kipekee ya kuzitumia na kulinda dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa.
Wito huo umetolewa na Afisa Usajili kutoka BRELA, Benedickson Willson wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara mkoani Tanga.
Willson amesema BRELA imeshiriki katika maonyesho hayo kwa lengo la kuwafikia wabunifu na wavumbuzi mbalimbali, kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kusajili kazi zao pamoja na kuwapatia huduma zinazohusiana na usajili wa ubunifu na mali miliki.
Amesema maonyesho hayo yanayofanyika kuanzia Agosti 15 hadi 24 mwaka huu ni fursa kwa wananchi kujifunza na kutambua namna ubunifu unavyoweza kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo ya mtu binafsi na Taifa.
“Watu wanachukulia ubunifu kwa mtazamo wa kawaida, lakini ubunifu ndiyo njia sahihi ya kuendeleza Taifa na kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,” amesema Willson.
Amesema usajili wa ubunifu unampa mbunifu au mvumbuzi haki ya kipekee ya kutumia kazi yake, huku ukimlinda dhidi ya watu wengine wanaoweza kutumia kazi hiyo bila ridhaa yake.
Kwa mujibu wa Willson, usajili wa alama ya biashara na huduma humwezesha mmiliki kulinda chapa yake dhidi ya bidhaa bandia zinazoweza kuingia sokoni kwa kutumia jina au alama yake bila ruhusa.
“Ukiwa umesajili alama yako ya biashara au huduma, unaweza kuzuia bidhaa bandia kutumia chapa yako bila kibali. Hii inakupa ulinzi wa kisheria na thamani ya kiuchumi ya chapa yako,” amesema.
Ameongeza kuwa usajili wa ubunifu pia unaweza kumwezesha mbunifu kutumia mali hiyo kama sehemu ya shughuli za kibiashara, ikiwamo kuingia makubaliano ya kibiashara na watu au taasisi nyingine.
Amesema mmiliki anaweza pia kuuza haki ya kutumia chapa au ubunifu wake kwa mtu mwingine kupitia makubaliano rasmi ya uhamishaji wa haki, hivyo kupata manufaa ya kifedha kutokana na kazi yake.
Willson amesema ubunifu unaohusisha teknolojia mpya una uwezo mkubwa wa kuwa mali yenye thamani endapo utasajiliwa na kulindwa ipasavyo.
Ametolea mfano ubunifu wa teknolojia zinazoweza kusaidia watu wenye changamoto mbalimbali, ikiwamo vifaa vinavyotumia akili bandia kufanya kazi zinazohitaji uwepo wa binadamu au teknolojia zinazoweza kuwasaidia watu wenye ulemavu wa kuona.
Amesema teknolojia kama hizo zinaweza kuwa na thamani kubwa kibiashara na kuwawezesha wabunifu kuingia katika makubaliano ya kibiashara na taasisi au kampuni ndani na nje ya Tanzania.
“Teknolojia mpya inayotatua changamoto fulani katika jamii inakuwa mali yenye thamani. Mbunifu anaweza kuitumia kibiashara au kuingia makubaliano na wadau mbalimbali kutokana na teknolojia hiyo,” amesema.
Aidha, amesema ubunifu unaweza kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa vijana endapo utasimamiwa na kulindwa kwa njia sahihi, huku akiwataka wabunifu kutokubali kazi zao zitumike bila kutambuliwa au kupata manufaa yanayostahili.
Ameeleza kuwa BRELA inaendelea kutumia maonyesho na majukwaa mbalimbali kuwafikia wabunifu na wavumbuzi ili kuwapatia elimu kuhusu taratibu za usajili na umuhimu wa kulinda kazi zao.
“Tunawakaribisha wabunifu, wavumbuzi na wataalamu wenye ubunifu wa aina mbalimbali kuja kupata huduma na elimu hapa. Lengo ni kuhakikisha ubunifu wao unatambuliwa, unalindwa na hatimaye unakuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa,” amesema.
Amesema ushiriki wa BRELA katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ubunifu unavyoweza kubadilishwa kuwa fursa ya kiuchumi na kuchangia katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.

More Stories
Dkt.Lingwanda apongeza ubunifu wa vijana katika maonesho ya NACTVET
TBS yataka biashara ya chakula,vipozi zisajiliwe
RC Tanga awaalika wananchi maonesho ya Elimu, Ujuzi