August 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Lingwanda apongeza ubunifu wa vijana katika maonesho ya NACTVET

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Dkt. Mwajuma Lingwanda, ametembelea banda la NACTVET katika maonyesho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea jijini Tanga, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ujuzi na ubunifu miongoni mwa vijana kwa ajili ya ushindani katika soko la ajira.

Katika ziara hiyo, Dkt. Lingwanda alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na NACTVET, pamoja na kushuhudia namna vijana wanavyotumia elimu, ujuzi na teknolojia katika kutengeneza bidhaa na kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu imeambatana na mashindano ya kitaifa ya ujuzi yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga, yakishirikisha vijana kutoka taasisi mbalimbali za elimu na mafunzo ya ufundi stadi.

Akizungumza kuhusu mashindano hayo, Dkt. Lingwanda amesema mashindano ya mwaka 2026 yamefikia hatua ya kitaifa baada ya kuanzia katika ngazi za vyuo, mikoa na kanda, hatua inayolenga kuwajengea vijana uwezo wa kushindana katika viwango vya juu zaidi.

Amesema jumla ya washiriki 46 wanashiriki katika mashindano hayo ya kitaifa yanayohusisha fani tisa .

Kwa mujibu wa Dkt. Lingwanda, mashindano hayo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, huku wakipewa fursa ya kuonyesha uwezo wao, kuongeza uzoefu na kuendeleza vipaji vyao.

Amesema awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika katika fani 15, lakini baada ya mchakato wa ushiriki, fani tisa ndizo zilizopata idadi kubwa ya washiriki na kufikia hatua ya kitaifa.

“Mashindano haya ni fursa muhimu kwa vijana kuonyesha uwezo wao, kuongeza uzoefu na kujiandaa kwa ushindani wa kitaifa, kikanda na kimataifa,” amesema.
Aidha, Dkt. Lingwanda amesema washindi watakaofanya vizuri watapata fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kikanda na kimataifa, hatua ambayo itawawezesha vijana kupima uwezo wao dhidi ya washiriki kutoka mataifa mengine.

Ametoa wito kwa wananchi, wanafunzi na wadau mbalimbali wa elimu kutembelea viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara na kujionea mashindano hayo pamoja na ubunifu unaofanywa na vijana, akisema ushiriki wa jamii utasaidia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa elimu ya ufundi na ujuzi katika maendeleo ya mtu binafsi na Taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora kutoka NACTVET, Jofrey Oleke, amesema mashindano hayo yamewaleta pamoja vijana wenye uwezo na vipaji mbalimbali kutoka taasisi za elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Ameeleza kuwa mchakato wa mashindano ulianza mwezi Juni mwaka huu baada ya matangazo kutolewa kwa vyuo mbalimbali nchini ili kuwapa wanafunzi fursa ya kushiriki.

Oleke amesema katika hatua ya kitaifa, kila fani ina washiriki watano waliotokana na washindi wa hatua zilizopita, isipokuwa fani ya ushonaji ambayo ina washiriki sita.

Ameongeza kuwa maandalizi ya mashindano yanaendelea vizuri, huku washiriki, waamuzi, majaji na wataalamu wanaoshiriki katika mchakato wa tathmini wakiwa tayari kutekeleza majukumu yao.

Akizungumzia ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya WorldSkills, Oleke amesema ujuzi ni nguzo muhimu katika kujenga nguvu kazi yenye uwezo na kuongeza kasi ya maendeleo ya Taifa.

Amesema WorldSkills ni mtandao unaounganisha nchi mbalimbali duniani katika kukuza na kuendeleza ujuzi, hivyo ushiriki wa Tanzania ni sehemu ya juhudi za kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira la ndani na kimataifa.

“Bila kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi, ni vigumu kwa nchi kufikia maendeleo yanayotarajiwa. Ni muhimu vijana kutoka shule za sekondari na vyuo kupewa fursa za kuendeleza vipaji na umahiri wao ili waweze kupata ajira, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa,” amesema.

Amesema viongozi na wadau wa WorldSkills wana wajibu wa kuhakikisha vijana wenye umahiri mkubwa wanatambuliwa, wanaendelezwa na kupewa fursa za kushindana katika viwango vya juu.