July 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TTCL yaonesha nguvu ya uchumi wa Kidijitali Sabasaba

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuonesha mchango wake katika kuharakisha utekelezaji wa uchumi wa kidijitali nchini kupitia matumizi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salama Mara baada ya kutembelea banda la shirika hilo katika Maonesho ya hayo ya sabasaba, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa amesema kuwa kupitia miundombinu hiyo ya kimkakati, shirika linaendelea kutoa huduma za mawasiliano zenye kasi kubwa, ubora wa hali ya juu na gharama nafuu ili kuwezesha wananchi, taasisi na sekta mbalimbali kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali unaolengwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema kuwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali hayawezi kufikiwa bila uwepo wa miundombinu imara ya mawasiliano inayowezesha upatikanaji wa intaneti ya uhakika na yenye kasi.

“Kwa kutumia Mkongo wa Taifa unaomilikiwa na kuendeshwa na TTCL, tunawezesha wananchi na taasisi kupata huduma za mawasiliano zenye spidi kubwa na kwa bei nafuu, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini,” amesema

Aidha amesema kuwa katika banda hilo wageni wanaotembelea watapata kufahamu huduma ya Supersonic Speed, iliyozinduliwa mwaka huu ikiwa ni huduma ya intaneti yenye kasi kubwa inayolenga kukidhi mahitaji ya watumiaji wa kisasa.

Marwa amesema huduma hiyo inatoa kasi ya intaneti ambayo inaifanya kampuni hiyo kuwa miongoni mwa watoa huduma wanaoongoza nchini katika utoaji wa intaneti yenye uwezo mkubwa kwa watumiaji wa majumbani na biashara.

Aidha, amesema TTCL imezindua FTTX Experience Center, kituo kinachoonesha namna teknolojia ya intaneti ya kasi inavyoweza kuboresha maisha ya kila siku kupitia matumizi ya smart home.

Amesema Kupitia kituo hicho, wananchi wanaoneshwa matumizi mbalimbali ya teknolojia ikiwemo kutazama video zenye ubora wa hali ya juu, kuimarisha usalama wa nyumba pamoja na kuendesha vifaa vya nyumbani kama friji, jiko na mashine za kufulia kwa kutumia mfumo wa mtandao.